Baadhi ya mashindano ya kale nchini
Na JOHN KIMWERE
MICHUANO ya kuwania taji la FKF Betway Cup awali ikifahamika kama Kombe la Ngao (GoTV) ni kati ya mashindano kongwe kabisa hapa nchini.
Pambano hilo lilibuniwa mwaka 1956 ambapo timu ya Mombasa Liverpool ilijvunia kushinda makala mawili ya kwanza mwaka 1956 na 1962.
Kisha Luo Union ilishinda mara mbili mfululizo hadi mwaka 1966 ilipodungwa mabao 4-2 na Mombasa Liverpool katika fainali na kunyang’anywa taji hilo. Kipute hicho kimejipatia sifa sufufu sawia na mikwaruzano ya FA Cup kule Bara Ulaya.
Hata hivyo mashindano hayo yamekuwa yakipewa majina tofauti kutokana na wadhamini. Baada ya kuanzishwa kipindi hicho yalibadilishwa jina na kuitwa FKF Presidents Cup yalipokosa mdhamini ambapo rais wa Kenya ndiye aliyekuwa akiwatuza washindi.
MOI GOLDEN CUP
Aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, Daniel Toroitich Arap Moi aliyezikwa wiki iliyopita, alikuwa mpenda michezo ambapo miaka ya ’80’ shindano hilo lilipewa jina lake na kuitwa Moi Golden Cup.
Kisha lilipewa jina jipya mwaka 2008 na kuitwa FKL Cup kabla ya kubadilishwa tena na kuitwa FKF Cup.
Katika hali ya kushangaza mwaka 2003, timu nne zilizokuwa zimetinga nusu fainali za shindano hilo zilijiondoa kutoka kipute hicho na kuendelea kucheza kivyake.
Hatua hiyo iliwalazimu waandalizi wa ngarambe hiyo kuzileta tena baadhi ya timu zilizokuwa zimebanduliwa nje.
Mwaka 2013 ndio Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) liliingia mkataba na GoTV na kuzindua ufadhili wa mashindano kuwa Kombe la Ngao (GoTV) kwa kipindi cha miaka mitano.
K’OGALO NA INGWE
Katika historia ya klabu mbili maarufu nchini, Gor Mahia FC na AFC Leopards maarufu kama Ingwe awali ikifahamika kama Abaluhya United kila moja imeshinda taji hilo mara kumi.
Mashindano hayo ya msimu huu yanaendelea yakifahamika kama FKFBetway Cup ambapo yanatazamiwa kuingia katika hatua ya 16 bora.
BINGWA 2019/2020
Bila shaka timu nyingi zinajiuliza mwaka huu nani atatwaa ubingwa wa taji la msimu huu? Je Gor Mahia maarufu K’Ogalo ama AFC Leopards mojawapo kati yazo itashinda taji la muhula huu?
Gor Mahia FC imepangwa kukabili Posta Rangers pia Ligi Kuu ya KPL.
Nayo AFC Leopards chini ya kocha, Anthony Kimani itakutanishwa na Ushuru FC inayocheza kipute cha Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL).
Gor Mahia ilipiga hatua hiyo ilipotoka chini mara mbili na kushinda Naivas FC kwa mabao 3-2 wiki iliyopita. Nayo AFC Leopards ilijikatia tiketi iliposhinda Elim FC bao 1-0. Posta Rangers ilishinda Tandaza FC nayo Ushuru ilijikatia tiketi ya kushiriki mechi za hatua hiyo ilipoangusha Transfoc mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kuagana sare bao 1-1.
MIAMBA WA SOKA
Dah! Wacha mambo ya Gor Mahia na AFC Leopards. Wapo watani wao pia ikiwamo Tusker ambayo imeshinbda taji hilo mara nne(4). Wengine wakiwa Sofapaka(3), Kariobangi Sharks (1), KCB (1), Bandari FC (2 ) pia Ulinzi Stars inayolenga kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza.
Sofapaka FC maarufu Batoto ba Mungu itacheza na Bandari nayo FC Talanta itapepetana na Kariobangi Sharks.
Kariobangi Sharks ilisonga mbele baada ya kuzoa ufanisi wa bao 1-0 dhidi ya Kenpoly FC. Nao wanasoka wa Sofapaka FC walikomoa Balaji EPZ kwenye mechi za raundi ya 32.
Bingwa wa taji hilo atatuzwa kitita cha Sh2 milioni na kutwaa tiketi ya kushiriki mechi za Kombe la Mashirikisho ya Afrika (CAF) baadaye mwaka huu. Nayo timu itakayomaliza ya pili itatia kibindoni Sh750,000 huku namba tatu ikipongezwa kwa Sh500,000