Manchester City siondoki mimi, asisitiza kocha Guardiola
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
KOCHA Pep Guardiola amesisitiza kuwa haondoki klabu ya Manchester City.
Aidha, Guardiola anaamini kuwa “ukweli utatamalaki”, baada ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya Bara Ulaya.
Mabingwa hao watetezi wa EPL walipewa adhabu hiyo na Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa) ya kutocheza Klabu Bingwa kwa miaka miwili. Pia walitozwa faini ya Sh3.2 bilioni.
Man-City imesema itakata rufaa katika Mahakama ya Kusikiza Kesi za Michezo (CAS).
“Tutakata rufaa. Mtu anapoamini hajakosea, ana haki ya kupigania ukweli,” Guardiola alisema. “Sisi ni watu tunaojua kazi yetu uwanjani, kile kinachofanyika nje ya uwanja hatuna mamlaka.”
Akizungumza Jumatano baada ya vijana wake kutesa West Ham 2-0 uwanjani Etihad kwenye mechi ya EPL, kocha huyo Mhispania aliongeza: “Tumezungumzia kile ambacho tunaweza kufanya hadi mwisho wa msimu, hasa kwa watu wanaopenda klabu hii. Tunacheza mechi kadri ya uwezo wetu. Tuko na vitu vingi vya kupigania.”
Alipoulizwa iwapo ataendelea kuwa kocha wa Man-City bila ya kuzingatia matokeo ya rufaa dhidi ya marufuku hiyo, alisema: “Wasiponitimua, nitakuwa hapa. Napenda klabu hii. Napenda kuwa hapa. Hii ni klabu yangu na nitakuwa hapa.
“Klabu hii inapasa kupigana na ninawaamini asilimia 100, kile wamefanya na wamenieleza. Hali hii haijatamatika na tutasubiri, lakini kabla ya uamuzi kufanywa wajibu wetu ni kucheza na kucheza na kucheza zaidi. Hicho ndicho kitu kitafanyika hapa.”
ManCity ilipatikana na hatia ya kuvunja sheria za kudhibiti fedha inazotumia, kwa kudanganya kiasi cha mapato yake kutoka kwa udhamini, kwa kipindi cha kati ya mwaka 2012 na 2016.
Ripoti ya bodi ya kuchunguza matumizi ya fedha za klabu (CFCB) pia iliongeza kuwa Man-City “ilikataa kushirikiana katika uchunguzi huo.”
Hata hivyo, Ijumaa iliyopita mabingwa hao watetezi wa EPL walisema kuwa “wamesikitishwa, lakini hawakushangazwa” na uamuzi huo wa “kuumiza” na kwamba watakata rufaa.
Hapo Jumatano, Afisa Mkuu Mtendaji, Ferran Soriano alisisitiza kuwa madai dhidi hayo “si kweli”.
Katika mchuano wa kwanza wa City tangu marufuku hiyo itangazwe, mabao ya Rodri na Kevin de Bruyne yalitosha kurejesha tabasamu klabuni.
, hasa baada pia ya kuchabangwa na Manchester United 1-0 kwenye nusu-fainali ya League Cup na kulemewa 2-0 dhidi ya Tottenham Hotspur ligini.
Mashabiki walionyesha kero lao kwa marufuku hiyo kwa kuimba nyimbo za kupinga Uefa katika kipindi cha kwanza. Baadhi ya mashabiki pia walibeba mabango yaliyokuwa na maandishi ‘Uefa ni muungano wa wakiritimba’ na “Uefa ni mafia’. Nyimbo za kuunga mkono kocha Pep Guardiola na mmiliki Sheikh Mansour zilikuwa nyingi.
Alipoulizwa kama rais wa klabu ya Barcelona Josep Maria Bartomeu anaunga mkono Uefa kuadhibu City, Guardiola alisema, “Sijui kama wananichunguza, lakini wananijua, si muhimu kunipeleleza…Msiropokwe sana Barcelona. Huo ndio ushauri wangu kwa sababu kila mtu hujipata katika hali ngumu. Tutakata rufaa na matumaini yetu ni kuwa tutashiriki Klabu Bingwa dhidi ya Barcelona.”