Habari

Brigid Kosgei amaliza katika nafasi ya pili Ras Al Khaimah Half Marathon

February 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 Brigid Kosgei amepoteza mbio kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 2018 baada ya kumaliza Ras Al Khaimah Half Marathon katika nafasi ya pili kwa saa 1:04:49 Ijumaa.

Raia wa Ethiopia Ababel Yeshaneh ameibuka mshindi kwa saa 1:04:31.

Kosgei, ambaye anajivunia kutimka Chicago Marathon mwaka 2019 kwa rekodi ya dunia ya saa 2:14:04 na hakuwa amepoteza mbio 11 mfululizo tangu Oktoba 2018, aliridhika katika nafasi ya pili kwa saa 1:04:49 mjini Ras Khaimah nchini Milki za Kiarabu.

Mkenya Joyciline Jepkosgei alishikilia rekodi ya dunia ya kilomita 21 ya saa 1:04:51, ambayo aliweka akishinda Valencia Half Marathon nchini Uhispania mwezi Oktoba mwaka 2017.

Kosgei alikuwa ametangaza azma yake ya kufuta rekodi ya Jepkosgei siku mbili kabla ya mashindano. Waliwekewa kasi na mkimbiaji mwanamume Geoffrey Pyego kutoka Kenya, ambaye majukumu yake yalikuwa kuhakikisha wanatimka umbali huo kwa saa 1:04:25.

Aliweka kasi ya juu ilioshuhudia kundi la kwanza la wakimbiaji tisa lililokuwa na Kosgei na Yeshaneh likikamilisha kilomita tano za kwanza kwa dakika 15:05, ambayo iliashiria mkimbiaji wa kwanza atafika utepeni kwa dakika 63:32.

Hata hivyo, kasi ilipungua kidogo katika kilomita tano zilizofuata wakikamilisha kilomita 10 za kwanza kwa dakika 30:17. Muethiopia huyo kisha aliongeza kasi na kufungua mwanya kidogo kati yake na Kosgei, ambaye aliziba mwanya huo.

Wawili hawa walikuwa bega kwa bega na kukamilisha kilomita ya 15 kwa dakika 45:39, ingawa Kosgei alionekana kuwa na maumivu. Kilomita moja baadaye, Yeshaneh alifungua mwanya tena na Kosgei hakuwa na jibu ila kupigania nafasi ya pili.

Kibiwot Kandie alinyakua taji la wanaume kwa dakika 58:57 akifuatiwa na Mkenya mwenzake Alexander Munyao (59:16) na Muethiopia Mule Wasihun (59:47) katika usanjari huo. Wakenya Alfred Barkach (59:49) na Vincent Raimoi (59:51) walifunga mduara wa tano-bora.