MWANAMKE MWELEDI: Alikuwa sauti kuu dhidi ya kansa na mtetezi wa jinsia
Na KEYB
ALIKUWA sauti kuu katika vita dhidi ya kansa ya matiti, haki za wanawake, demokrasia na mwunganisho wa kitaifa.
Ni kazi ambayo Bi Mary Onyango aliifanya kwa ukakamavu na kujitolea huku akihudumu katika nyadhifa kuu za usimamizi kwa miongo miwili unusu.
Baada ya kugundulika kuugua kansa ya matiti mwaka wa 1999, alishirikiana na Bi Julia Mulaha ambaye alikuwa mwathiriwa wa kansa, kuanzisha mpango wa Kenya Breast Health Programme – shirika la utetezi na kutoa msaada kwa waathiriwa wa kansa.
Bi Julia alifariki mwaka wa 2003, na kumuacha Bi Onyango kuhudumu kama mkurugenzi mtendaji katika shirika hilo ambapo baadaye, lilipanua huduma zake na kuhusisha pia huduma kwa waathiriwa wa virusi vya HIV/AIDS.
Kabla ya kufariki mwaka wa 2012 kutokana na maradhi ya kansa, Bi Onyango alikuwa amehudumu kwa kipindi cha miaka 25 katika nyadhifa mbali mbali za uongozi.
Aliwahi hudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), ambapo wakati huu alihusika katika miradi tofauti ya kurejesha amani miongoni mwa jamii zinazoishi katika eneo la Mlima Elgon.
Aidha, alikuwa mwanachama wa bodi za usimamizi katika mashirika tofauti ya ufadhili na mashirika ya kijamii nchini Kenya. Pia, alikuwa mwanachama wa Taasisi ya Mahasibu wa umma walioidhinishwa nchini (Institute of Certified Public Accountants of Kenya).
Bi Onyango alisomea biashara (Uhasibu) katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Baadaye alisomea shahada ya uzamifu katika masuala ya kibiashara (Kifedha) kutoka Chuo Kikuu cha Maastricht, nchini Uholanzi. Halikadhalika, alisomea shahada nyingine ya uzamifu katika masuala ya afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Aliendesha kampeni za Kenya Kwanza, zilizonuiwa kuhakikisha uchaguzi mkuu huru wa kitaifa 2012/13, na pia kuepuka ghasia za baada ya uchaguzi sawa na zilizoshuhudiwa katika uchaguzi mkuu wa kitaifa wa 2007/2008. Katika haya yote alijitahidi kuhakikisha kwamba matukio ya ghasia wakati wa uchaguzi nchini hayashuhudiwi tena.