Habari

Muthama akataa picha ya Musyoka uhasama kati yao ukizidi

February 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

PIUS MAUNDU na BENSON MATHEKA

UHASAMA wa kisiasa kati ya kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Seneta wa Machakos, Bw Johnstone Muthama ulidhihirika wazi mbunge huyo wa zamani wa Kangundo alipokataa kupigwa picha pamoja na Bw Musyoka.

Bw Muthama na Bw Musyoka walikuwa wamehudhuria mazishi ya aliyekuwa afisa wa chama cha Kanu katika Kaunti ya Machakos, Bw Muthama alipokataa mwaliko wa kupigwa picha pamoja na Bw Musyoka na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua.

Kisa hiki kilitokea baada ya Bw Musyoka na Dkt Mutua kuzika tofauti zao na kuamua kushirikiana.

Bw Musyoka aliwaalika wanasiasa wengine waliohudhuria mazishi hayo kupigwa picha kuadhimisha muafaka wake na Dkt Mutua lakini Muthama akataa kujiunga nao.

Waziri msaidizi Wavinya Ndeti, Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jr, wabunge Victor Munyaka (Machakos Mjini) na Daniel Maanzo (Makueni) na aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile waliamka kwa haraka na kupanda jukwaani.

Waombolezaji walipaza sauti kumtaka Muthama kujiunga na wanasiasa hao lakini akakataa katakata na ikabidi Musyoka kumuita ajiunge nao.

Hata hivyo, Bw Muthama alimpuuza na hata kuwaelekezea kidole wanasiasa waliokuwa wakimhimiza kusimama kuwaonya.

Bw Musyoka aliachana naye na wakapigwa picha huku Muthama akionekana kutotishika.

Kulingana na wadadisi, hiyo ilikuwa ishara kwamba Bw Muthama hafurahishwi na mwelekeo wa kisiasa ambao Bw Musyoka anachukua pamoja na ushirika wake na Dkt Mutua.

Dkt Mutua alikuwa amemtaja Bw Muthama kama mmoja wa wandani wa Bw Musyoka ambao alikuwa amewasamehe alipoamua kushirikiana na kiongozi huyo wa chama cha Wiper.

Tangu mwaka wa 2013, Muthama na Mutua wamekuwa wakizozana, gavana huyo akimlaumu bwanyenye huyo kwa kuhujumu serikali yake.

Ingawa Muthama alikuwa mmoja wa wandani wa karibu wa Bw Musyoka, walitofautiana majuzi kufuatia misimamo yao kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI).

Bw Muthama alitumia hafla hiyo kukosoa BBI aliosema itagawanya Wakenya zaidi.

Mwaka jana, Musyoka alikanusha madai ya Bw Muthama kwamba alikuwa akizungumza na Naibu Rais William Ruto kwa lengo la kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Muthama alikuwa amesema alikuwa akiongoza mazungumzo ya wawili hao kuungana.

Hata hivyo, Bw Musyoka alisisitiza kuwa yuko nyuma ya Rais Uhuru Kenyatta kuunga BBI.

Bw Musyoka alimtaka kuacha kujitenga na kuungana na wanasiasa wengine kuunga BBI.