JAMVI: Ni nani atafaidika kwa maridhiano ya Mutua na Kalonzo?
BENSON MATHEKA na PIUS MAUNDU
MARIDHIANO kati ya Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka na Gavana wa Machakos Alfred Mutua yalichochewa na tamaa ya wawili hao walio na azma ya kugombea urais na sio kwa manufaa ya eneo la Ukambani, wadadisi wanasema.
Hata hivyo, wanasema maridhiano hayo yanamfaidi zaidi Dkt Mutua kuliko Bw Musyoka ikizingatiwa kuwa gavana huyo anahudumu kipindi cha pili na atahitaji kujijenga katika ngazi ya kitaifa.
Ingawa wawili hao walisema walizika tofauti zao ili kufanikisha maendeleo eneo la Ukambani, hisia za wengi ni kuwa hatua yao huenda ikawa ya muda tu hasa baada ya kuibuka kuwa walishinikizwa na Rais Kenyatta kuzika tofauti zao.
“Kwa kuwa walisukumwa kupatana, huenda maridhiano yao yasidumu kwa muda mrefu. Kila mmoja angali na azima ya kugombea urais na kwa vile wanatarajia baraka za Rais Kenyatta, hawakutaka kumkaidi. Ni muda tu utakaoamua iwapo ushirikiano wao mpya utadumu,” asema mdadisi wa siasa za Ukambani, Joshua Kiilu.
Anasema Bw Musyoka anataka kuonekana kuwa anathibiti ngome yake ya Ukambani ilhali kwa wakati huu, Mutua anataka kuungwa mkono na madiwani wa Wiper katika bunge la kaunti ya Machakos ambao amekuwa akilaumu kwa kuhujumu ajenda zake.
“Kila mmoja ana ajenda zake za kibinfsi anazotaka kutimiza. Kwa upande wa Bw Musyoka, anataka kuonekana kwamba ngome yake ya Ukambani iko nyuma yake anapotafuta uungwaji mkono na viongozi wengine kitaifa ilhali Mutua anataka kuungwa mkono na madiwani wa Wiper kufanikisha ajenda zake katika kaunti ya Machakos,” aeleza Bw Kiilu.
Walipotangaza maridhiano yao katika mazishi ya mfanyabiashara Mulwa Kang’aatu wiki hii, Dkt Mutua alimtaka Bw Musyoka kuwaagiza madiwani wa chama chake cha Wiper ambao ndio wengi katika bunge la kaunti ya Machakos kuacha kumpiga vita, wito ambao Bw Musyoka alikubali.
“Viongozi wa Maendeleo Chap Chap na Wiper wanapaswa kuungana katika bunge la kaunti ili wazungumze kwa sauti moja,” Bw Musyoka alisema hatua ambayo wadadisi wanasema ni ushindi wa kwanza kwa Dkt Mutua kufuatia maridhiano hayo.
Dkt Mutua alisema yuko tayari kumuunga mkono Bw Musyoka kugombea urais iwapo wakazi wa Ukambani watahisi kuwa ni makamu rais huyo wa zamani anayefaa kupeperusha bendera ya jamii yao kitaifa naye Bw Musyoka akasema atakuwa akimpigia debe Dkt Mutua kote nchini kuimarisha umaarufu wake.
Wadadisi wanasema ushirikiano huo ni ushindi kwa Dkt Mutua anapojiandaa kwa siasa za kitaifa baada ya kuhudumu kama gavana kwa mihula miwili.
“Pia Mutua amefaulu kumzima aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama wa chama cha Wiper ambaye amekuwa akimlaumu kwa kuhujumu miradi yake ya maendeleo. Muthama ametofautiana kisiasa na Bw Musyoka na Dkt Mutua hakupoteza nafasi hiyo kujifaidi,” aeleza Bw Kiilu.
Ingawa baadhi ya wanasiasa wa Wiper wanasema kuwa hatua hiyo inapiga jeki azima ya Bw Musyoka ya kugombea urais, wadadisi wanasema itabidi afanye kazi ya ziada kuwavuta magavana Charity Ngilu wa Kitui, Kivutha Kibwana wa Makueni na Bw Muthama upande wake.
“Ushirikiano wake na Dkt Mutua sio mwisho wa upinzani eneo la Ukambani. Itabidi atafute muafaka na Bi Ngilu na Profesa Kibwana ambao wana mwelekeo tofauti wa kisiasa,” asema Bi Susan Nyiva, mwanaharakati wa siasa eneo la Ukambani.
Kulingana na Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Machakos Joyce Kamene, handisheki ya Dkt Mutua na Bw Musyoka inaonyesha ukomavu wao kisiasa. Mwanasiasa huyo anahisi kuwa muafaka wao umepiga jeki safari ya Bw Musyoka ya kuelekea Ikulu.
Wanaohisi kwamba ushirikiano wa Dkt Mutua na Bw Musyoka sio mwisho wa mgawanyiko wa kisiasa eneo la Ukambani wanataja tofauti zilizozuka wakati wa mjadala kuhusu Mpango wa Maridhiano BBI wakisema umezua mipasuko zaidi.
Ilichukua umahiri na ukakamavu wa mfanyabiashara Peter Muthoka ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta kuwaleta pamoja viongozi wa Ukambani waliokuwa wamepanga mikutano tofauti.
Magavana wa kaunti tatu za eneo hilo walikuwa wameandaa mkutano kaunti ya Kitui naye Bw Musyoka na chama cha Wiper walikuwa wameandaa wao kaunti ya Makueni. Baada ya Bw Muthoka kukutana nao, waliamua kuhudhuria mikutano yote miwili kuanzia uliokuwa Kitui.
Hata hivyo, Bw Kibwana amejitenga na mkutano wa Makueni ambao Bw Musyoka na Dkt Mutua wanasema utafanyika Machi.
Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr anaamini kwamba jinsi hali ilivyo, mzozo baina ya viongozi wa Ukambani utaendelea.
“Sio lazima tukubaliane kila wakati. Hata hivyo, hatufai kutusiana na kugombana hadharani,” alisema.
Wadadisi wanasema nyota ya Dkt Mutua inaweza kung’aa zaidi iwapo atawashawishi magavana Ngilu na Kibwana kuiga mfano wake na kuungana na Bw Musyoka.
Inasemekana Bw Muthoka alitekeleza wajibu mkubwa kupatanisha Dkt Mutua na Bw Musyoka.
Wadadisi wanasema Dkt Mutua alifanya uamuzi unaofaa ikizingatiwa kuwa ana nafasi ya kukwea ngazi kisiasa kufikia hadhi ya Bw Musyoka.