• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kabras Sugar watinga nusu-fainali Kenya Cup huku Bulls na Kisumu zikishushwa ngazi

Kabras Sugar watinga nusu-fainali Kenya Cup huku Bulls na Kisumu zikishushwa ngazi

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) mwaka 2016 Kabras Sugar wamejikatia tiketi ya kushiriki mechi za nusu-fainali msimu huu wa 2019-2020 baada ya kulipua Nondescripts 52-6 mjini Kakamega, Jumamosi.

Wanasukari wa Kabras walilemea washikilizi hao wa rekodi ya mataji mengi ya Kenya Cup (17) kupitia miguso ya Lawrence Buyachi, Charlton Mokua, Brian Tanga, Paul Abuto, George Nyambua, Asuman Mugerwa na Jone Kubu. Ntabeni Dukisa alichangia mikwaju mitano naye Kubu akafunga mkwaju mmoja.

Vijana wa kocha Henly Du Plessis, ambao wako juu ya jedwali la ligi hiyo ya klabu 12, wamefikisha alama 70 kwa hivyo hawawezi kufikia nambari tatu Homeboyz.

Mabingwa watetezi KCB wataungana na Kabras katika nusu-fainali wakipiga sare katika mchuano wao wa mwisho wa muda wa kawaida dhidi ya Homeboyz mnamo Februari 22. Wanabenki wa KCB, ambao wako alama moja nyuma ya Kabras, walijiweka pazuri kuingia awamu hiyo baada ya kupepeta Menengai Oilers 43-13 uwanjani Ruaraka hapo Jumamosi katika mechi za raundi ya 16.

Timu mbili za kwanza katika muda wa kawaida zitatinga nusu-fainali moja kwa moja na pia kuwa wenyeji wa mechi hizo. Homeboyz pia ilijihakikishia nafasi ya tatu katika msimu wa kawaida baada ya kulipua Western Bulls 56-6 mjini Kakamega.

Timu zitakazokamilisha muda wa kawaida katika nafasi ya tatu, nne, tano na sita zitawania tiketi mbili za mwisho za kushiriki nusu-fainali. Impala Saracens, Oilers, Mwamba na Nakuru wako katika vita vikali vya kumaliza ndani ya sita-bora. Licha ya kupoteza dhidi ya Mwamba 15-11 Jumamosi, Impala ilipata alama moja ya bonasi inayoihakikishia nafasi ya nne katika muda wa kawaida.

Bulls na Kisumu wanaoshikilia nafasi mbili za mwisho wametemwa kutoka Ligi Kuu, ingawa bado wanasalia na mechi ya kufunga msimu wikendi ijayo.

Matokeo (Februari 22):

KCB 43-13 Menengai Oilers

Mwamba 15-11 Impala Saracens

Kabras Sugar 52-6 Nondescripts

Kenya Harlequin 33-12 Nakuru

Western Bulls 6-56 Homeboyz

Kisumu 5-38 Blak Blad

You can share this post!

Ingwe yang’aria Sofapaka tena mechi ya ligi KPL

MWANASIASA NGANGARI: Waziri aliyezindua huduma ya simu za...

adminleo