Makala

MATHEKA: Ushirikiano kati ya Mutua, Kalonzo uwe wa nia njema

February 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ya kuzika tofauti zao inaashiria mwamko mpya wa siasa za eneo la Ukambani ikiwa kweli ushirikiano wao una nia njema.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakilaumiana kila wakati na kusema kweli, tofauti zao na za viongozi wengine, zimevuruga maendeleo eneo la Ukambani.

Ni matumaini yangu kuwa magavana wengine wa kaunti za Ukambani; Charity Ngilu wa Kitui na Kivutha Kibwana wa Makueni, watazika tofauti zao na Bw Musyoka na kuunganisha jamii ya Wakamba ambayo ni ya tano kwa idadi ya watu nchini.

Ikizingatiwa kuwa siasa za Kenya huegemea misingi ya kijamii, mchango wa Wakamba katika siasa za Kenya hauwezi kupuuzwa. Hata hivyo, ni umoja wa viongozi unaowezesha jamii yoyote ile kuwa na usemi katika uongozi wa taifa hili. Ni wazi kuwa tofauti za viongozi wa Ukambani zimefanya miradi mingi ya maendeleo ambayo ingefaidi wakazi kukwama.

Miradi kama ya Konza City, mradi wa makaa ya mawe kaunti ya Kitui na Bwawa la Grand Falls Dam ambalo lingegharimu zaidi ya Sh200 bilioni ni baadhi ya miradi iliyokwama kwa sababu viongozi wa eneo la Ukambani hawakuweza kuzungumza kwa sauti moja.

Ikiwa basi viongozi hao wanajali maslahi ya wakazi, ni lazima waungane kwa nia njema na kudumisha umoja wao hadi baada ya uchaguzi mkuu ujao. Nasema hivi kwa sababu sio mara ya kwanza ya viongozi wa Ukambani kutangaza wameungana na kisha kutofautiana kwa sababu ambazo wanaweza kusuluhisha wenyewe.

Kwa mfano, Dkt Mutua alijiunga na siasa kupitia chama cha Wiper cha Bw Musyoka kabla ya wawili hao kutofautiana na kuanza kurushiana lawama hadharani hadi Mutua akaunda chama chake cha Maendeleo Chap Chap.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bi Ngilu na Bw Kibwana waliungana na Bw Musyoka katika muungano wa NASA kabla ya magavana hao kujitenga na Bw Musyoka na kuungana na Dkt Mutua kumlimbikizia lawama makamu wa rais huyo wa zamani.

Matokeo yalikuwa ni madiwani wa Wiper ambao ndio wengi kulemaza shughuli katika serikali za kaunti hatua ambayo iliathiri huduma.

Kwa maoni yangu, na nilimsikia Dkt Mutua akisema haya, tofauti za viongozi hazifai kufanya wananchi wasio na hatia kukosa huduma. Akiwa mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa eneo la Ukambani ambaye anajulikana kwa sifa zake za kidiplomasia nchini na kimataifa, Bw Musyoka anafaa kutumia kila mbinu kurejesha uhusiano wake na Bw Kibwana na Bi Ngilu kwa manufaa ya wakazi wa eneo la Ukambani.

Ikiwa lengo la viongozi hao ni kufanikisha maendeleo wanavyodai, wanafaa kuungana kwa msingi huo alivyosema Dkt Mutua alipoungana na Bw Musyoka kuhudhuria mazishi ya mfanyabiashara mmoja kaunti ya Machakos wili jana.

Kiongozi ni yule anayeweza kuunganisha jamii, sio tu kumchagua, bali pia kufanya maamuzi muhimu. Ningewashauri viongozi wote wa Ukambani kutumia matokeo ya sensa ya mwaka kama msingi wa kukutana, kuichanganua na kuweka mikakati itakayohakikisha jamii imepata haki inayostahili kitaifa wanavyofanya viongozi wa maeneo mengine.