Makala

WARUI: TSC ikipanga mafunzo ya walimu kiholela hayatafaulu

February 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANTO WARUI

MPANGO wa mafunzo ya walimu ambao unatarajiwa kupitishwa kwa wao wote kote nchini ni mzuri na ambao unaweza kuwa na manufaa mengi katika sekta ya elimu.

Hata hivyo, mafunzo hayo yasipopangwa vizuri na kutekelezwa kwa uangalifu itakuwa ni kazi ya kupotezea walimu muda na pesa zao.

Tume ya kuwaajiri walimu (TSC) imesema kuwa mafunzo hayo yanatarajiwa kufikia walimu wapatao 472,000 wa shule za umma pamoja na zile za kibinafsi.

Mafunzo haya ambayo TSC inasema kuwa ni ya lazima kwa kila mwalimu yatatekelezwa kwa awamu sita na yatamgharimu mwalimu sh6,000 kila mwaka.

TSC imewekeana mkataba na vyuo vikuu vinne nchini ambavyo ni: Kenyatta University, Riara University, Mount Kenya University na Kenya Education Management Institute (KEMI) ambavyo vimepewa jukumu la kuwafunza walimu wote.

Kulingana na Tume ya kuwaajiri walimu, mafunzo haya yatatolewa kupitia njia ya mtandao na ile ya moja kwa moja. Walimu wanatarajiwa kujiandikisha kisha kulipia mafunzo hayo kupitia shuleni ambako wanafunza.

Kuna walimu wengi nchini ambao wamejisajili na TSC lakini bado hawana kazi. Walimu hawa watajiandikisha kupitia shule gani? Ni wapi ambako TSC inatarajia walimu hao wapate pesa za mafunzo ambayo inasema ni ya lazima?

Siku za hivi majuzi tumeona Wizara ya Elimu ikitoa mafunzo ya mtaala mpya wa elimu (CBC) kwa walimu.

Mafunzo hayo yamekuwa yakifanyiwa katika kumbi fulani ambapo ungekuta walimu wote wa kaunti-ndogo wamekusanyika katika ukumbi mmoja.

Matokeo yake ni kuwa ukumbi ulijaa zaidi ya walimu mia tano wengine wakilazimika kukaa nje. Ni kweli kusema kuwa walimu wengi waliohudhuria mafunzo hayo hawakufaidika kamwe.

Jambo kama hili, pale ambapo wahadhiri wanahitaji kutoa mafunzo ya moja kwa moja, litakuwa ni changamoto kubwa kwa walimu kuweza kupata mafunzo yafaayo.

Tume ya kuwaajiri walimu (TSC)tayari imeshasema kuwa mafunzo haya yataanza mwezi Aprili 2020.

Huku ukiwa umebakia mwezi mmoja tu, TSC haijatoa mwelekeo ufaao kwa walimu ili waweze kujisajili.

Aidha haijashirikisha washikadau wengine kama vile walimu wa shule za wamiliki binafsi na chama cha walimu cha KNUT.

Tayari tumesikia KNUT ikitoa malalamishi yake kupinga mpango wa mafunzo hayo ikisema kuwa haijashirikishwa katika maandalizi yake.

Malalamishi kama hayo yanaashiria kuwa kutakuwa na pingamizi kutoka kwa baadhi ya walimu hasa ikizingatiwa kuwa TSC inawalazimisha walimu kushiriki mafunzo ilhali haiwalipii chochote.

Ikiwa TSC inataka mpango huu wote ufaulu, basi haina budi kuweka mikakati ifaayo zaidi na kushirikisha wadau wote. Mafunzo haya yakipangwa kiholela itakuwa kazi ya kupotezea walimu muda na pesa zao.