Michezo

Mvutano wa msajili, FKF sasa wahatarisha Kenya

February 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

MSAJILI wa Michezo, Rose Wasike amejipata katika hali ngumu kueleza ni kwa nini amezembea kutoa mwelekeo kwa mashirika ya michezo kuzingatia sheria mpya ya michezo nchini.

Wasike yuko motoni hususan kuhusiana na Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kwa kukosa kuliwezesha kutimiza mahitaji ya sheria mpya ya michezo nchini.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo Jumanne mbele ya Jopo la Kutatua mvutano Michezoni (SDT), ambapo FKF imeshtaki msajili huyo aliyepiga marufuku uchaguzi wa shirikisho hilo hadi liwe tayari kuendesha shughuli kuambatana na sheria mpya ya spoti.

Wakili wa Wasike, Martin Munene aliulizwa na mwenyekiti wa SDT, John Ohaga aeleze kwa nini mvutano huo umechukuwa zaidi ya mwaka kutatuliwa.

Munene alikuwa amefahamisha jopo hilo kwamba FKF ilikuwa ikiendesha shughuli hizo, bila kuzingatia agizo la Wasike.

“Mvutano huu ulianza mwezi Mei 2018. Ofisi yako ilikuwa na wakati wa kutosha kuelekeza FKF ihakikishe imefuata masharti yaliyo kwenye sheria mpya ya spoti,” alisema.

Akaongeza: “Kulingana na sheria mpya, mashirika ya michezo yalipaswa kuandikisha kaunti zote nchini kuambatana na sheria mpya na kufanya uchaguzi wake kulingana na sheria mpya za spoti 2018. Ofisi yake imekuwa ikiongojea nini tangu wakati huo?”

Munene kadhalika alieleza kuwa FKF imepuuza maagizo ya Wasike na kuendelea na mipango ya kuandaa uchaguzi wake kuanzia mashinani, licha ya kukumbushwa mara mbili.

Awali, wakili Charles Ouma, akiwakilisha timu za Bondeni United na Chepterit kwenye kesi hiyo, alidai kwamba zaidi ya klabu 300 zimezuiliwa kushiriki kwenye zoezi hilo, kwa madai kwamba hazijajiandikisha kama wanachama.