Oparanya alaumiwa kwa kutelekeza majukumu yake katika kaunti
Na KEN WAMASEBU
MADIWANI watatu wa Kaunti ya Kakamega sasa wanadai Gavana Wycliffe Oparanya anajishughulisha sana na siasa za kitaifa na mpango wa maridhiano (BBI) huku akiitelekeza kaunti na wakazi wake.
Wamemtaka ajirudi na aanze kuzingatia kazi yake.
Madiwani hao wa chama cha ANC Farouk Machanje wa wadi ya Isukha Kusini, Walter Andati wa Butsotso Kusini na Joab Mwamto wa Shieywe walisema Gavana amepuuza majukumu yake.
“Anajihusisha na siasa za kitaifa na BBI badala ya kuwahudumia wananchi,” akasema Bw Andati.
Walisema katika hotuba yake ya nne kwa kikao cha madiwani katika bunge la kaunti, Oparanya alishindwa kuangazia masuala muhimu.
Bw Machanje alisema Oparanya hana mamlaka kuelekeza madiwani na bunge la kaunti ambalo wajibu wake ni kuupiga msasa utawala wake.
“Anatulazimishia mambo sisi madiwani jinsi ambavyo tunafaa kutumia pesa na raslimali, lakini pia ameshindwa kupambana na ufisadi unaogubika doa utawala wake,” akasema Bw Machanje.
Machanje alisema hospitali ya rufaa katika kaunti hiyo haijakamilishwa jinsi inavyofaa.
“Kaunti inapata msaada wa maendeleo wa kiasi cha Sh227 milioni kila mwaka kutoka kwa Benki ya Dunia, lakini ni Sh50 milioni pekee ambazo zimetengewa maendeleo ikiwa ni kinyume na matarajia ya mpango huo,” akasema.
Viongozi hao walisema serikali ya kaunti iliwakosea wafanyabiashara kwa kubomoa vibanda vya biashara.
Walisikitika Sh37.5 milioni zilizoidhinishwa kwa ajili ya kutumika kupeana mikopo kwa wafanyabiashara wa miji mbalimbali katika kaunti hiyo, hazijatolewa.
Biashara zilikuwa na leseni na stakabadhi muhimu kutoka kwa serikali ya kaunti, lakini vibanda na maduka yalibomolewa bila ya wafanyabiashara kupewa notisi za kuwaandaa wagure; tumeshindwa kuwaelezea hili tukio,” akasema Bw Mwamto.