Kioja abiria jini akipotelea hewani!
Na Charles Ongadi
MAGANYAKULO, KWALE
BODABODA wa hapa alilazimika kuacha pikipiki yake kwenye steji na kutimka mbio za mguu niponye baada ya abiria wa kike aliyembeba kutoweka ghafla.
Kulingana na bodaboda mwenzake aliyekuwa akimfuata hatua chache nyuma, alimuona mwenzake akimbeba abiria wa kike.
Wote walikuwa wameanza safari pamoja kuwafikisha abiria wao walikokuwa wakienda. Alisema hata yeye alijipata amechanganyikiwa muda mchache baadaye alipomwona mwenzake akiendesha pikipiki bila abiria ilhali hakuwa amesimama kumshusha.
“Kweli kapanda yule abiria wa kike lakini alivyotoweka ghafla akiwa kabebwa na mwenzangu ingali kitendawili kwangu,” alisimulia jamaa huyo huku akionekana kuchanganyikiwa.
Jamaa alipogundua abiria wake alikuwa ametoweka, alisimamisha pikipiki na akatimua mbio kama aliyepandwa na mzuka.
Lakini hatua ya haraka iliyochukuliwa na wasamaria wema na bodaboda wa eneo hili ilifanikiwa kumzuia bodaboda huyo kuendelea kutimka mbio.
Bodaboda huyu aliishia kupoteza fahamu kwa muda ila alirudia hali yake ya kawaida na kusimulia wenzake yaliyomsibu.
“Ama kwa kweli nilimkuta binti yule mrembo katika steji akichat na akaniomba nimfikishe beach lakini muda mfupi baada ya kuanza safari yetu nilipomwangalia na side mirrow sikumwona na ndipo nikajipata nimechanganyikiwa,” alisimulia bodaboda huyo huku akiwaomba wenzake kumsindikiza hadi kwao.
Alipofika mbele ya wazazi wake, bodaboda huyo aliapa kutofanya tena kazi ya bodaboda huku akiwaomba wazazi wake kumtafutia kazi nyingine ya kufanya.
Siku mbili baadaye, alionekana akielekea shule ya karibu ya kiufundi na ikasemekana aliamua kujifunza kazi ya useremala.