Michezo

Christine Ongare anyakua tiketi ya kuchapana ndondi katika michezo ya Olimpiki 2020

February 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

CHRISTINE Ongare amenyakua tiketi ya kuchapana ndondi katika michezo ya Olimpiki 2020 baada ya kulima raia wa Uganda Catherine Nanziri katika mechi ya kufa kupona ya kutafuta nambari tatu ya Bara Afrika mjini Dakar, Senegal, Jumamosi.

Ongare alishinda Nanziri katika uzani wa kilo 51 (Flyweight) kwa alama 5-0 katika pigano ambalo lingeenda upande wowote kwa sababu mabondia hawa walionekana kusukumiana makonde mazito.

Ongare alifuzu kutoka kitengo hiki pamoja na Roumaysa Boualam (Algeria) na Rabab Cheddar (Morocco) waliomaliza katika nafasi mbili za kwanza, matawalia.

Mkenya huyo alianza kampeni yake kwa kunyamazisha Ornella Havyarimana (Burundi) 5-0 na kuingia nusu-fainali baada ya kulaza Modestine Munga Zalia (DR Congo) 5-0 kabla ya kupigwa na Cheddar 5-0 katika nusu-fainali.

Mabondia wengine wanawake kutoka Kenya Elizabeth Andiego (Middleweight), Evelyne Akinyi (Lightweight), Elizabeth Akinyi (Welterweight) na Beatrice Akoth (Featherweight) walibanduliwa nje mapema.

Kenya pia itawakilishwa katika masumbwi ya wanaume mjini Tokyo na bondia mmoja wa kiume Nick Okoth. Nahodha huyo wa timu ya taifa ya ndondi mjini Dakar aliridhika na medali ya fedha baada ya kulemewa na Mzambia Everisto Mulenga katiia fainali ya uzani wa “Featherweight” Jumamosi.

Rayton Okwiri (Middleweight), Hassan Shaffi Bakari (Flyweight), Elly Ajowi (Heavyweight), Joseph Shigali (Lightweight), Boniface Mugunde (Welterweight), Humphrey Ochieng’ (Light Heavyweight) na Fredrick Ramogi (Super Heavyweight) walibanduliwa nje katika awamu mbalimbali za mashindano.