RIZIKI: Mwanadada anayesema ajira haihitaji mtu kujiuza kimwili
Na SAMMY WAWERU
KATIKA kikao cha mahojiano na Magdalene Wanjiru katika mkahawa mmoja kiungani mwa jiji la Nairobi, kila anapozungumza anatabasamu.
Unapotangamana naye, ni mwingi wa bashasha na mcheshi ajabu.
Hata hivyo, ni tabasamu inayoficha mengi, hasa mazito aliyopitia kusukuma gurudumu la maisha.
Kwa ufafanuzi, tabasamu ni kuonyesha uso wa furaha unaoambatana na haja ya kucheka bila kutoa sauti wala kufungua kinywa, na ni hulka anayokumbatia kujifariji.
Mwanadada Wanjiru alizaliwa ipatayo miaka 36 iliyopita, Gatundu, Kaunti ya Kiambu, ambako pia ni nyumbani kwao.
Ni msomi, na anasimulia kwamba katika shule ya msingi na upili alitia bidii za mchwa, akapita mtihani licha ya kuwa wazazi hawakujiweza vile kimapato.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta, KU, kilichoko pembezoni mwa Thika Superhighway, akasomea taaluma ya Mawasiliano na Teknolojia (IT).
“Nilifuzu kwa Shahada mnamo 2009, nikajiunga na vijana kutafuta ajira,” Wanjiru anafichua.
Nchini Kenya iwapo kuna jambo linalohangaisha vijana, liite ukosefu wa ajira. Ni finyu, na zilizoko zinaendea wachache ambao ‘jamaa zao’ wana ushawishi serikalini au katika kampuni na mashirika mbalimbali.
Ni changamoto ambazo Wanjiru ambaye ni Mkatoliki na mcha Mungu alipitia kwa muda wa miaka mitatu mfululizo, baada ya kuhitimu chuo kikuu.
“Nilikuwa nikituma maombi ya kazi katika kampuni na mashirika mengi, vitengo vya IT. Kuna walionialika kupigwa msasa na wengine maombi hayakujibiwa,” anasimulia.
Pandashuka alizopitia, zilikuwa kioo kilichoonesha mahangaiko wanayopitia vijana. Hata hivyo, kando na kuhitajika kuwa na tajiriba ya miaka kadhaa, kilichomuuma moyo ni baadhi ya ‘maagizo’ aliyotakiwa.
Anakumbuka barabara kana kwamba ilikuwa jana tu, kisa kimoja ambapo alifua dafu kuajiriwa katika kampuni moja jijini Nairobi. Alitakiwa kuanza gange hiyo siku kadhaa baada ya kupokea barua ya kuajiriwa.
Malipo yalikuwa ya kuridhisha, lakini siku mbili kabla kuripoti, bosi aliyempa kazi alimualika katika mkahawa mmoja jijini anachotaja kama “kujadili majukumu aliyotwikwa”. La kushangaza, mwaliko huo ulijiri majira ya jioni.
“Nilijua wazi mazungumzo yangehusu majukumu yangu na kupata ushauri,” anaeleza.
Anahadithia kwamba baada ya kukutana na bosi huyo, mjadala uliendelea barabara na hata akatia saini kandarasi ya kuajiriwa.
Kabla kumuaga, Wanjiru anadokeza kwamba hakujua kulikuwa na hitaji lingine alilopaswa kuhitimisha, na ndilo lilimuatua moyo zaidi.
“Alikuwa amekodi chumba, ambalo alisisitiza tungekesha ‘nilipie’ kupata nafasi ya kazi aliyonipa. Nilivyomhepa, ilikuwa kwa neema ya Mungu, kazi iliyobarikiwa haipatikani kwa njia hiyo,” anafafanua, akiongeza kusema kuwa hakujutia kupoteza kazi hiyo.
Ni tukio lililomhuzunisha, swali lililomtinga likiwa “Kazi inayopatikana kwa njia ya haki, kwa nini niipate kwa kufanya mapenzi na bosi?” Hakupata majibu, ila aliamini Mungu ndiye hufungua njia.
Visa vya aina hiyo si vigeni si tu hapa nchini, ila pia katika mataifa mengine ulimwenguni na kulingana na Padre Paul Wachira, vijana wanapaswa kuwa na misimamo dhabiti na imara wanapotafuta kazi. “Wasitekwe na majaribu ya aina hiyo, pamoja na mengine maovu. Mwenyezi Mungu hutakasa kazi zinazopatikana kwa njia faafu na ya kuridhisha,” anashauri mtumishi huyo.
Katika safari ya kuendelea kusaka kazi, Magdalene Wanjiru anaiambia ‘Taifa Leo’ kuwa miezi kadhaa baadaye, alipata ajira Kaunti ya Kericho.
Ilihusisha kozi aliyosomea, na anasema aliifanya kwa muda wa miaka minne mfululizo.
Masaibu ya kumezewa mate na baadhi ya bosi zake yaliibuka tena, na anasema ndiyo yalichangia kutema kazi aliyofanya.
Isitoshe, waliomtamani walikuwa wameoa.
Wanjiru anasisitiza kama Mkristu na zaidi ya yote mcha Mungu, ikiwa kuna jambo asiloweza kufanya ni kuwa katika uhusiano wowote haramu.
Ni unyanyapaa unaozingira wanawake wengi, kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza, baadhi ya walio kwenye ndoa wakiishia kutumbukia katika mtumbwi huo.
Ni muhimu kujua ni vitendo vinavyotia wahusika katika hatari ya maambukizi ya maradhi ya zinaaa.
“Watu wakithamini heshima, usakaji na upataji wa kazi utakuwa na uwazi na uadilifu,” Wanjiru anasema. Pia, dhuluma katika maeneo ya kazi zitapungua kwa kiasi kikuu, kijana huyo akipendekeza kampuni na mashirika yakaze kamba kuimarisha sheria mahususi na uadilifu miongoni mwa viongozi kazini.
Kwa sasa Magdalene akiendelea kutafuta ajira, anafanya kazi za mitandao kama vile kusadia wafanyabiashara kutafuta soko la bidhaa. Ni shughuli inayohusisha kushawishi wachangiaji wa mitandao ubora wa bidhaa.