Michezo

Shujaa yaridhika kuzoa alama tatu Los Angeles Sevens

March 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume ya Kenya, Shujaa, iliambulia alama tatu katika duru ya tano ya Raga ya Dunia mjini Los Angeles, Marekani, mnamo Machi 1 usiku.

Vijana wa kocha Paul Feeney walizoa alama hizo baada ya kupoteza 29-24 dhidi ya Scotland katika mechi ya kutafuta nambari 13 na 14.

Walianza kampeni ya Los Angeles kwa kulemewa 31-5 na Afrika Kusini mnamo Februari 29 usiku katika mechi ya Kundi B ambayo William Ambaka alifunga mguso wa kufutia machozi.

Kenya kisha iliamka katika mchuano wa pili ilipokung’uta Ireland 29-12 kupitia miguso ya Vincent Onyala (mitatu), Oscar Dennis na Collins Injera kabla ya kuaibishwa 24-0 na Canada itakayoandaa duru ya sita hapo Machi 7-8.

Matokeo hayo yalisukuma Shujaa kuwania nafasi 9-16 ambapo ililimwa 28-19 na Samoa katika robo-fainali ya Challenge Trophy ikipata alama zake katika mchuano huo kupitia kwa miguso ya Onyala (miwili) na Samuel Oliech (mmoja). Daniel Taabu alipachika mikwaju ya miguso miwili.

Kichapo hicho kiliteremsha Shujaa katika mechi ya kuwania nusu-fainali ya kuorodheshwa kutoka nafasi ya 13 hadi 16. Ililipua Wales 29-5 na kujiondoa katika hatari ya kuvuta mkia tena baada ya kufanya hivyo katika duru ya nne mjini Sydney nchini Australia mapema Februari.

Vijana wa Feeney walizamisha Wales kupitia kwa miguso ya Ambaka, Oliech, Dennis, Oscar Ouma na Jeff Oluoch. Oliech na Taabu walifunga mkwaju mmoja kila mmoja katika mchuano huo.

Shujaa kisha iliingia mchuano wa kuamua nambari 13 na 14 dhidi ya Scotland ambapo ilipata miguso kutoka kwa Ambaka, Billy Odhiambo, Oliech na nahodha Andrew Amonde, lakini ikalemewa dakika ya mwisho. Oliech alifunga mikwaju miwili na mchuano huo.

Baada ya duru hiyo, Kenya imesalia katika nafasi ya 11 duniani kwa alama 29.

Mabingwa wa Cape Town na Hamilton New Zealand wanaongoza ligi hii ya mataifa 15 kwa alama 93, nne mbele ya washindi wa Dubai na Los Angeles Afrika Kusini nao washindi wa Sydney Sevens Fiji wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 72. Ufaransa (alama 67), Uingereza (64), Australia (62), Marekani (60), Argentina (53), Ireland (45) na Canada (40) zinafunga mduara wa 10-bora.

Scotaland ni ya 12 sako kwa bako kwa alama 29 na Kenya nayo Samoa ni ya 13 alama moja nyuma. Wales inakamata nafasi ya 15 ya kutemwa. Imezoa alama 11. Japan, ambayo ilialikwa kushiriki duru nne za kwanza, ina alama tisa nayo Korea ina alama moja baada ya kualikwa mjini Los Angeles na kuvuta mkia.