Michezo

Kocha Ouma ataja kikosi cha Harambee Starlets kinachoelekea Istanbul

March 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA David Ouma ametaja kikosi chake cha mwisho kitakachoelekea mjini Istanbul hapo Machi 3 asubuhi kwa mashindano ya kimataifa ya Turkish Women’s Cup 2020 yatakayodumu wiki moja.

Wachezaji 12 walikuwa katika timu ya Harambee Starlets iliyokanyaga kila mpinzani ikitwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) nchini Tanzania miezi mitatu iliyopita.

Baadhi ya wachezaji hao ni mshambuliaji matata wa Thika Queens Mwanahalima Adam, kiungo stadi Jentrix Shikangwa (Wiyeta Girls) na beki Dorcas Shikobe (Oserian).

Starlets itakuwa timu ya kwanza kabisa kutoka Bara Afrika kushiriki mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 2018.

Makala ya mwaka 2020 yamevutia Uturuki, Kenya, Hungary, Venezuela, Hong Kong, Romania, Uzbekistan, Northern Ireland, Turkmenistan na Chile.

Inamaanisha kuwa bingwa mpya atajulikana mwaka huu kwa sababu timu ya pili ya Ufaransa (France B) ambayo ilitawala makala yaliyopita, haikuingia makala haya ya tatu.

Starlets inatumia kipute hicho kujipiga msasa kabla ya kuanza kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AWCON) 2020 dhidi ya Tanzania mnamo Aprili.

 

Kikosi cha Starlets kinachoelekea Uturuki

Makipa – Judith Osimbo, Monica Odato, Stella Ahono;

Mabeki – Vivian Nasaka, Lucy Akoth, Nelly Sawe, Foscah Nashivanda, Dorcas Shikobe, Dorcas Shiveka, Lydia Akoth;

Viungo – Sylvia Makungu, Sheril Angachi, Jentrix Shikangwa, Janet Budi, Rachael Muema, Mercy Airo, Topistar Situma;

Washambuliaji – Stella Anyango, Jane Njeri, Mwanahalima Adam, Purity Anyetu.