Habari

Majeshi ya Somalia na Jubaland yapigana vikali karibu na Kenya

March 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MANASE OTSIALO

MAPIGANO makali yalichacha Jumatatu karibu na mji wa Mandera kati ya wanajeshi wa serikali ya Somalia na wale wa eneo la Jubba.

Wanajeshi wa Somalia walikuwa wakijaribu kumkamata waziri wa ulinzi wa Jubba aliyetoroka jela mapema mwaka huu, Abdirashid Janan anayejificha Kenya.

Majeshi ya serikali hizo mbili yalikabiliana vikali kwa siku nzima kwenye mpaka wa Kenya na Somalia, wakazi wa upande wa Kenya wakilazimika kufunga biashara zao na pia shule zikasitisha masomo.

Tangu Bw Janan alipowasili Kenya, hali ya taharuki mjini Mandera imekuwa ikitanda na kuwalazimu baadhi ya wakazi kutoroka makwao wakihofia mapigano kuzuka.

Wakati walipolemewa na wanajeshi wa Somalia, wale wa Jubba walikimbilia Kenya ambako walipewa hifadhi katika kituo cha polisi cha Mandera mjini ambacho kilikuwa chini ya ulinzi wa KDF.

Hata hivyo, haikubainika iwapo Bw Janan alisalia hotelini ambako amekuwa akikaa mjini Mandera ama alifichwa katika kambi ya kijeshi ya Mandera.

Waziri huyo amekuwa akijificha katika hoteli moja mjini Mandera tangu Januari 30 baada ya kuhepa kutoka jela alikokuwa akizuiliwa na serikali ya Somalia tangu Agosti 31, 2019.

Tangu alipoingia hapa Kenya, taharuki imekuwa ikitanda mjini Mandera ambako amekuwa akilindwa na majeshi ya Jubba ambayo yanaungwa mkono na serikali ya Kenya dhidi ya uvamizi wa majeshi ya Somalia.

“Sisi tulijua kwamba machafuko haya yangetokea lakini serikali yetu ilikataa kimakusudi kumkamata waziri huyo na kumrejesha kwao au kumkabidhi kwa utawala wa Somalia,” akasema mkazi wa Mandera kwa jina Ali Hassan.

Maafisa wa usalama wa ngazi za juu wa Kenya walikimbilia kambi ya jeshi mjini Mandera huku mapigano yakichacha. Kamanda wa polisi wa Mandera Jeremiah Kosiom alionekana akisindikizwa hadi kwenye kambi hiyo chini ya ulinzi mkali.

Kituo cha polisi cha Mandera nacho kilisalia mahame baada ya vita kuchipuka huku maduka mengi na shule mjini Mandera zikifungwa.

Mhudumu wa afya katika hospitali ya rufaa ya Mandera nayo alieleza Taifa Leo kwamba hawakuwa wamepokea manusura yeyote wa vita hivyo.