• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Miundomsingi Githurai yaendelea kuimarishwa kutatua msongamano wa magari

Miundomsingi Githurai yaendelea kuimarishwa kutatua msongamano wa magari

Na SAMMY WAWERU

KUIMARIKA kwa miundomsingi kama vile barabara kunatajwa kama njia mojawapo inayoashiria maendeleo katika eneo, na hilo si tofauti na mtaa wa Githurai ulioko kiungani mwa jiji la Nairobi.

Awali, mtaa huo ulipotajwa ulihusishwa na visa vya uhalifu na kila aliyenuwia kuutembelea alionywa.

Hata ingawa husemekana soko kamilifu halikosi sarakasi, mtaa huo katika siku za hivi karibuni umeonekana kukua kwa kasi.

Tangu Thika Superhighway – barabara kuu inayounganisha mji wa Thika na jiji la Nairobi – izinduliwe mnamo 2009 na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, mtaa huo ulio pembezoni mwa barabara hiyo unajivunia maendeleo mbalimbali.

Ikilinganishwa na miaka ya awali, idadi ya watu sasa imeongezeka mara dufu, baadhi yao wakiingilia uwekezaji. Unapozuru Githurai, biashara zilizonoga zinaendeshwa saa 24 sawa na siku nzima, ishara kuwa uchumi unakua.

Misongamano ya watu na magari, ni taswira usiyokosa kushuhudia kila saa eneo hilo, hasa katika barabara inayounganisha Githurai na Mwihoko.

Mbali na ujenzi wa barabara ya Eastern Bypass, itakayoungana na Thika Superhighway ikikamilika, serikali kuu kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Kiambu inaendelea kuimarisha barabara za mashinani katika kile kinachoonekana kama kutafuta suluhu ya kupunguza misongamano ya magari.

Ujenzi wa kituo cha reli cha Githurai, kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni, umejiri na kuimarishwa kwa barabara kadhaa. Mradi huo unaopaniwa kuwa na magarimoshi ya abiria na mizigo, umeshinikiza utengenezaji wa barabara inayounganisha Githurai na Mwiki.

Ni kupitia kituo hicho, ambapo barabara kadha zitakazoungana na Thika Superhighway, zinaundwa, mfano ukiwa inayopitia kitongoji cha Toezz, Mwiki Primary na Kwa D.O.

Matingatinga yanaendelea kuchimba, huku mawe yakimwagwa wanakandarasi wakijikakamua kuweka lami.

“Barabara tunazolenga zikikamilika misongamano ya magari itapungua kwa kiasi kikuu,” akasema diwani wa wadi ya Githurai Mwiki, Bw James Mburu.

Akipigia upatu ujenzi huo, MCA huyo amesema anatazamia biashara kuimarika, ikizingatiwa mtaa huo unapatikana katika kaunti ya Kiambu ambayo ni tajika katika shughuli za kilimo na kiungani mwa jiji la Nairobi.

“Biashara unazoona zikifunguliwa kama vile uuzaji wa nguo, zimebuni nafasi za ajira hasa kwa vijana,” akasema, pia akitaja huduma za tuktuk na pikipiki miongoni mwa sekta zitakazofaida pakubwa.

Eneo hilo lina zaidi ya bodaboda 2,000 na tuktuk zisizopungua 300. Hayo yakijiri, usalama unaendelea kuimarisha na asasi husika.

You can share this post!

TALAKA: Madiwani wa kike Lamu wawalaumu akina mama wapendao...

Papa Francis akatiza likizo kwa sababu ya mafua

adminleo