Kizazi kipya cha nzige kitavamia Kenya – FAO
Na VALENTINE OBARA
SHIRIKA la Chakula na Kilimo (FAO) linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa, limeonya kwamba nchi itashuhudia shamblio la kizazi kipya cha nzige wakati wakulima wanapojiandaa kwa msimu wa upanzi.
Nzige wamevamia zaidi ya kaunti 20 kufikia sasa na kusababisha uharibifu mkubwa kwa mimea ya kilimo na lishe ya mifugo.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, FAO ilisema kuna wasiwasi kuhusu jinsi nzige walioanguliwa majuzi wameanza kukomaa na kujikusanya katika makundi mapya.
Hali hii inaleta hofu ya uhaba wa chakula ambayo inaweza kuhatarisha hali ya maisha ya wananchi siku zijazo, kwa mujibu na shirika hilo.
“Nzige wanaendelea kutaga mayai katika kaunti za kaskazini na kati ya nchi ambapo kuna makundi mapya yaliyoanza kukomaa katika siku za hivi majuzi,” FAO ilisema kwenye taarifa.
Kando na wale wanaoanguliwa humu nchini, inahofiwa kuna makundi mapya yanayoweza kushambulia nchi kutoka Somalia kwani wameonekana katika maeneo ya Barbera na Burao yaliyo kaskazini nchini humo.
Imetabiriwa Kaunti za Marsabit na Turkana ndizo zitakuwa na idadi kubwa zaidi ya wadudu hao waharibifu.
Mnamo Jumatatu, Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya alisema mpango wa serikali kupambana na nzige unaendelea vyema.
Hata hivyo, alikiri kuna changamoto kukabiliana na shambulio jipya hasa kuhusiana na wadudu watakaotoka Somalia kwani hakuna juhudi zinazoendelezwa kuwaangamiza katika nchi hiyo kwa sababu ya vita vilivyopo.
“Tuna mpango kamili kuhusu jinsi ya kukabiliana na nzige. Mpango huo utadumu hadi Juni,” akaeleza.
Serikali hutegemea unyunyizaji dawa za kuua nzige kutoka angani na vilevile ardhini ili kuua nzige waliokomaa pamoja na kuharibu mayai yao.
Bw Munya alisema licha ya nzige kuonekana wakiendelea kusambaa, serikali inaamini itafanikiwa katika mipango yake ya kuzuia janga.
Wakati huo huo, Serikali ya Uingereza imefungua kituo maalumu cha kutabiri mienendo ya nzige kwa teknolojia za setilaiti jijini Nairobi.
Kituo hicho kimefunguliwa katika makao makuu ya Shirika la Utabiri na Utumizi wa Tabia Nchi linalosimamiwa na IGAD (ICPAC).
Wataalamu katika kituo hicho watatumia data kutoka kwa idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Uingereza kutabiri safari za nzige ili kusaidia wadau kuweka mikakati ya mapema kuwaangamiza kabla wawasili wanakoelekea.