• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
RIZIKI: Kutoka uchuuzi wa vitambaa hadi mmiliki wa duka la vipuri vya motokaa

RIZIKI: Kutoka uchuuzi wa vitambaa hadi mmiliki wa duka la vipuri vya motokaa

Na SAMMY WAWERU

AAMKAPO Selina Wanjiku anasema huanza siku yake kwa hupiga dua kwa Mwenyezi Mungu akimshukuru kwa kumjalia uhai.

Anasema hiyo ndiyo ratiba yake kila siku.

Mola, ambaye hujaalia kila mmoja kulingana na mapenzi yake, amemfanyia makuu maishani.

La muhimu zaidi ni kuwa hai kuiona siku inapopambazuka. “Kuiona siku inapokucha ni kwa neema ya Mungu, tuna kila sababu kumshukuru,” Wanjiku anasema.

Ipatayo miaka sita hivi iliyopita, kijana huyo anaiambia Taifa Leo kwamba alihangaikia jijini Nairobi akitafuta kazi.

Hiyo ilikuwa baada ya kuchoshwa na maisha ya mashambani, miaka miwili baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE.

Kwa kuwa wazazi wake hawakujiweza vile kimapato, ili ajiunge na taasisi ya juu ya elimu ajiendeleze kimasomo, Wanjiku hakuwa na budi ila kukita kambi Nairobi.

“Nilitamani kupata kazi hata kama ni ya uyaya, niweze kujiimarisha na kusaidia wazazi wangu pia,” anasema.

Mwaka 2013 na ambao ulikuwa mwaka wa uchaguzi mkuu chini ya katiba ya sasa iliyoidhinishwa 2010 msichana huyo alitua Nairobi, akalakiwa na kaka yake.

Anasimulia kwamba, kakaye ambaye ana mke pia, alimsaidia kukithi baadhi ya mahitaji yake, kama vile kumpa nauli kusafiri jijini kutafuta kazi.

“Nilikuwa radhi hata kuosha vyoo,” aelezea.

Ikizingatiwa kuwa alikuwa na cheti cha kufuzu KCSE pekee, anasema mengi ya mashirika, kampuni, na hata maduka yalihitaji awe na kozi, kama vile ya tarakalishi.

Baada ya kuhangaika kwa mwaka mmoja, Selina Wanjiku anasema aliingilia uchuuzi wa vitambaa vya kupiga chafya na soksi, katika kitovu cha jiji, ndicho CBD. Ni gange yenye mapato, hasa ukiwa na bidhaa zenye soko la haraka.

Hata hivyo, kizingiti kikuu kilikuwa maafisa wa halmashauri ya jiji, maarufu kama kanju, ambao mwanadada huyo anasema walimhangaisha ikikumbukwa kuwa alikuwa angali mdogo kiumri.

Anasimulia, si mara moja, mbili au tatu alijipata kukwaruzana nao, kiasi cha kuzuiliwa kwenye gari tamba karibu siku nzima.

“Wakati mwingine ningeangua kilio, nikiwarai waniachilie nina watoto wanaonitegemea, ingawa sikuwa nao. Baadhi walinihurumia,” anakumbuka.

Licha ya changamoto hizo, hakujipata kufikishwa kortini, kwenye simulizi yake akimshukuru Mungu kwa dhati kwa kumuepushia hayo.

Miaka miwili baadaye, Wanjiku anasema alikuwa ameweka akiba mapato yaliyomfanikisha kufungua duka la bidhaa.

“Mnamo 2016, niliweka biashara ya kuuza vipuri vya motokaa na pikipiki,” adokeza.

Ni hatua iliyomgharimu kima cha zaidi ya Sh200,000 akisema kiasi fulani cha mtaji huo alipigwa jeki na chama cha ushirika (Sacco) alichokuwa akiweka akiba, akapata mkopo.

“Ninahimiza vijana kukumbatia uwekaji akiba. Ukilipwa Sh5 tenga Sh1 au Sh2 ziweke kama akiba kwenye shirika lolote la kifedha la chaguo lako,” ashauri kauli inayotiliwa mkazo na mtaalamu Peninah Sianoi.

“Ni muhimu kuweka akiba kwa sababu ya siku za usoni. Haijalishi kazi unayofanya, bora unaweza kujipanga,” Sianoi anaeleza, akishauri haja ya kuchagua vyama bora vya ushirika kwa kutathmini historia yavyo.

Kwenye kauli hiyo, anamaanisha mashirika ya kifedha ambayo yamesajiliwa kisheria na yenye mikakati kabambe katika utendakazi.

Mtaalamu huyo wa masuala ya kiuchumi anaonya kuwa kuna baadhi ya vyama vya ushirika, Sacco ambavyo hufunguliwa kwa minajili ya kutapeli, hivyo basi haja ipo kuvipiga msasa kabla kujiunga navyo.

Uuzaji wa vipuri, kulingana na Wanjiku, 26, ni biashara yenye mapato ya kuridhisha ikipata usimamizi mzuri, ikiwa ni pamoja na kuelewa mahitaji ya wateja. Amewekeza eneo la Mwiki, Kasarani, Kaunti ya Nairobi, na anasema hivi karibuni anapania kufungua duka jingine.

Ni kazi anayosema aliitamani akiwa kwenye gange ya uchuuzi.

Kabla kuingilia biashara yoyote ile, unashauriwa kufanya utafiti wa kina, kujua soko, na utakapotoa bidhaa, jambo ambalo kijana Selina Wanjiku anasema alilifanya kwa umakinifu.

Amebuni nafasi ya kazi kwa mhudumu mmoja, anayemsaidia kusambaza vipuri na vifaa vingine vya magari. Ili kuimarisha jitihada zake, anasema anajiendeleza kimasomo, ambapo anasomea kozi ya biashara katika chuo kimoja jijini.

“Nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa makuu aliyonitendea, ndio maana siku huanza kwa dua na kuihitimu kwa dua pia,” anasema, akihimiza vijana wenzake kutolaza damu.

Anasema ndoto wanazoazimia zitaafikiwa iwapo watatia shime na bidii, muhimu zaidi ikiwa kushirikisha Mungu katika kila hatua.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Si wakati wote neno ‘kuhusu’...

UFISADI: Waandamanaji Kisumu watisha kufunga ofisi za EACC

adminleo