• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Mashabiki wa Harambee Stars kuingia mechi ya Comoros bila malipo Kasarani

Mashabiki wa Harambee Stars kuingia mechi ya Comoros bila malipo Kasarani

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Kenya wataingia uwanjani Kasarani bila malipo kushuhudia mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2021 dhidi ya Comoros hapo Machi 25 kwa hisani ya kampuni ya bahati nasibu ya Betika.

Shirikisho la Soka Kenya (FKF) lilisema Alhamisi kuwa limefanya mapatano na Betika kuondoa ada ya langoni kwa mchuano huo wa Kundi G.

“Mkataba wa Sh3 milioni kati ya FKF na Betika utawezesha mashabiki kuingia uwanjani bila malipo. Hii ni sehemu ya mipango ya Betika kuinua soka ya Kenya katika mashinani na pia ngazi ya kitaifa,” FKF imesema.

Afisa Mkuu wa Biashara Betika John Mbatiah aliongeza, “Tunafurahia sana kusaidia Harambee Stars. Tunaamini kuwa tangazo hili litasaidia kutoa mchango muhimu ambao Stars inahitaji ili iweze kuimarisha nafasi ya kufuzu kushiriki AFCON 2021.”

Rais wa FKF Nick Mwendwa alipongeza ushirikiano huo akisema utapatia Harambee Stars motisha na mamilioni ya mashabiki wa soka kote nchini.

“Tunaomba Wakenya wajitokeze kwa wingi kushabikia Harambee Stars inapotafuta tiketi kushiriki AFCON kwa mara ya pili mfululizo. Tunaamini kuwa kuondolewa kwa ada ya langoni itawezesha maelfu ya mashabiki kufika uwanjani na pia kupatia wachezaji mazingira mazuri ya kupata matokeo mema,” alisema.

Wanavisiwa wa Comoros wanaongoza kundi hilo kwa alama nne baada ya kuchapa Togo 1-0 mjini Lome na kulazimisha sare tasa dhidi ya miamba Misri mjini Moroni.

Kenya na Misri zimezoa alama mbili kila mmoja.

Stars ilikaba Misri 1-1 mjini Alexandria na kuandikisha matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo uwanjani Kasarani.

Togo inavuta mkia kwa alama moja. Timu mbili za kwanza katika makundi yote 12 zitaingia AFCON 2021 nchini Cameroon.

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi 98 Mukuru waokolewa na kupewa ufadhili wa masomo

Ruto asema nia ya wabaya wake ni kumpaka tope

adminleo