• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
DINI: Tumia thawabu yako kama mama kuwalea watoto wako kwa wema

DINI: Tumia thawabu yako kama mama kuwalea watoto wako kwa wema

Na FAUSTIN KAMUGISHA

“NANI kama mama?”

“Mama namthamini kwa thamani isiyo kifani.” Ni baadhi ya misemo ya Kiswahili inayokutwa katika kanga au leso za akinamama.

Misemo hii inadokeza kwa namna fulani heshima anayopewa mama. Umama si heshima tu bali ni kazi.

Tunaweza kuwa na Litania fupi ya Mama. Mama ni mzazi. Mama ni mlezi. Mama ni mwalimu. Mama ni mbeba uhai. Mama ni mbeba mimba. Mama ni mtia moyo. Mama ni mfariji.

Mama ni mshauri. Mama ni mzaa chema. Mama ni mzaa mkubwa.Mama ni nguzo. Mama ni mchakalikaji.

Kuna aliyetoa litania ya mama hivi: “Mama ni jiko pindi unapokuwa na njaa. Mama ni hospitali ukiwa mgonjwa. Mama ni ukumbi wa sherehe, pindi unapofurahi. Mama ni saa ya kukuamsha pindi unapolala. Mama ni dua pindi unapokuwa mbali.” Kwa kifupi mama ana sifa ya huruma.

Mateso ya mtoto ni mateso ya mama. Mwanamke Mkanaani alimwambia Yesu, “Unihurumie, Bwana, Mwana wa Daudi, Binti yangu anasumbuliwa sana na pepo mbaya” (Mathayo 15:22).

Mahangaiko makubwa ya huyu mwanamke Mkananayo yanaonekana wazi. Yeye hakusema, umhurumie binti yangu, ila unihurumie mimi; kwa sababu mateso ya mtoto ni mateso ya mama pia. Na ili kuvuta huruma yake zaidi, alimfungulia daktari kidonda na mapana na marefu ya ugonjwa; mapana na marefu aliposema, anasumbuliwa sana na pepo mbaya; aina ya ugonjwa ni kusumbuliwa pepo mbaya.

Kumbuka mateso ya Mtakatifu Augustino yalikuwa pia mateso ya mamake Monica. Mwishowe, wote wakawa watakatifu (Monica na Augustino).

Nakubaliana na Sarah Orne Jewett aliyesema, “Maadamu una mama, bado wewe unaendelea kuwa mtoto.” Maombezi ya mama yana nguvu.

Lakini kuna matumizi mabaya ya nguvu ya umama. Somo lifuatalo linasema ukweli wote.

“Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, “Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji… kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana, akakichukua kwa mamaye” (Mathayo 14:6-11).

Mama huyu ambaye alimshauri vibaya mwanawe aliitwa Herodia. Mwanawe aliitwa Salome. Herodia hakutoa mfano mzuri kwa mwanawe.

“Usiwe na hofu kwamba watoto hawakusikilizi; kuwa na hofu kwamba kila mara wanakutazama,” alisema Robert Fulghum.

Salome alimtazama mama yake ambaye hakutoa mfano mzuri.

Mama huyu aliolewa na wanaume wawili ambao ni ndugu kwa nyakati tofauti. Herode alimuoa mwanamke huyu ambaye alikuwa ni mke wa ndugu yake aliyeitwa Filipo. Yohane alimwambia, “Si halali kwako kuwa naye.”

Maneno hayo yalikuwa ni mwiba uliochoma moyo wa Herodia. Akatafuta wakati mzuri wa kumwondoa Yohane Mbatizaji kutoka kwenye ramani ya dunia.

Katika kisa hiki tunaona makosa ambayo wazazi hufanya.

Upendo ni shamba la mtoto. Lakini si watoto wote wanafaidi matunda kutoka katika shamba hili.

“Ni rahisi kujenga watoto shupavu kuliko kukarabati watu wazima waliovunjika,” alisema Frederick Douglass.

Malezi ya watoto ni muhimu. Kuna mtoto aliyebandika kikaratasi kwenye mlango wa chumba cha wazazi wake chenye maneno haya: “Mungu usiwape wazazi mtoto mwingine kwa kuwa waliyenaye hawajui kumlea vizuri.”

Katika mazingira kama hayo, kuna mambo ambayo yanakuwa hayako vizuri.

Katika benki ya kumbukumbu ya mtoto kunaingizwa jambo baya. Kosa la kuwatumia watoto kama vyombo na si lengo la kuwa mzazi.

Herodia alimtumia binti yake Salome kama chombo cha kuonyesha chuki yake kwa Yohane Mbatizaji.

“Kuwa baba mwema na mama mwema kunahitaji wazazi kuacha mahitaji yao na tamaa zao kwa ajili ya mahitaji ya watoto. Kama matokeo ya sadaka ya namna hii, wazazi waangalifu huendeleza ubora wa tabia na hujifunza kuweka katika matendo ukweli usiofutika uliofundishwa na Mwokozi mwenyewe,” alisema James E. Faust.

You can share this post!

RIZIKI: Hiki kinaweza kuyumba Mungu akakujalia kile

Msajili vyama atoa onyo kali kwa usitishaji wa uchaguzi

adminleo