• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Harambee Starlets yafundishwa soka na Chile kwa kupigwa 5-0

Harambee Starlets yafundishwa soka na Chile kwa kupigwa 5-0

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets imekubali kichapo katika mechi yake ya pili ya soka ya kimataifa ya Turkish Women’s Cup baada ya kuaibishwa 5-0 na Chile katika mechi ya Kundi B iliyogaragazwa Jumamosi uwanjani Gold City mjini Alanya nchini Uturuki.

Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) walikuwa wamechapa Northern Ireland 2-0 katika mechi yao ya ufunguzi Machi 4.

Walijipata chini bao moja dakika ya tisa pale kiungo Yessenia Lopez baada ya kupokea mpira kutoka kwa mshambuliaji wa Sevilla, Yanara Aedo.

Kiungo Karen Araya alitonesha kidonda cha Kenya kwa kuongeza bao la pili dakika ya 23.

Mvamizi matata Mwanahalima ‘Dogo’ Adam alipata nafasi nzuri ya kupatia goli kabla ya mapumziko alipovuta shuti, lakini kipa wa klabu ya Paris Saint-Germain Christiane Endler alikuwa macho kuondosha hatari hiyo.

Mambo ya Kenya yaliharibika kabisa ilipojisababishia penalti dakika ya 55 na kufungwa kupitia kwa Aedo kabla ya Araya kutikisa nyavu tena dakika ya 60.

Shuti la Cote Urrutia liligonga mwamba dakika ya 64 kabla ya Paloma Lopez kufuma wavuni bao la tano dakika ya 83.

Chile iliingia mchuano huu ikipigiwa upatu kunga’ara, hasa kwa sababu inaorodheshwa katika nafasi ya 36 kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Kenya, ambayo itamenyana na Black Queens ya Ghana katika mechi yake ya mwisho ya makundi Machi 10, inapatikana katika nafasi ya 133 duniani.

Starlets ya kocha David Ouma inatumia mashindano haya ya timu nane kujipiga msasa kabla ya kuvaana na Tanzania katika mechi yake ya raundi ya kwanza ya kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Bara Afrika (AWCON) baadaye mwaka 2020.

Kenya na Tanzania zitapepetana mwezi Aprili, huku mshindi akikutana na mshindi wa mechi nyingine ya raundi ya kwanza kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sao Tome & Principe katika raundi ya pili ili kuingia AWCON 2020.

Ratiba na matokeo ya Turkish Women’s Cup 2020:

Machi 4

Hungary 2-1 BIIK Kazygurt (Kundi A)

Romania 4-1 Hong Kong (Kundi A)

Chile 3-0 Ghana (Kundi B)

Kenya 2-0 Northern Ireland (Kundi B)

Machi 7

Hong Kong na Hungary (Kundi A)

BIIK Kazygurt na Romania (Kundi A)

Kenya 0-5 Chile (Kundi B)

Northern Ireland na Ghana (Kundi B)

Machi 10

Romania na Hungary (Kundi A)

Chile na Northern Ireland (Kundi B)

Ghana na Kenya (Kundi B)

BIIK Kazygurt na Hong Kong (Kundi A)

  • Tags

You can share this post!

ODM yatisha kumng’oa Dkt Ruto

Mathare United, Tusker zasajili ushindi

adminleo