Habari

Corona kuua mamilioni

March 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

HUENDA homa hatari inayosababishwa na virusi vya Corona ikaua mamilioni ya watu duniani katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, huku ripoti mpya ikifichua kuwa takriban watu nusu milioni wataangamia nchini Amerika pekee.

Hayo yalifichuka wakati idadi ya watu wanaoambukizwa kote ulimwenguni ikiongezeka katika nchi mbalimbali.

Kulingana na ripoti hiyo iliyowasilishwa na Chama cha Hospitali Nchini Amerika (AHA) Februari, ugonjwa huo unaenea kwa kasi zaidi duniani kuliko inavyoripotiwa.

Chama hicho kilisema kuwa, inakadiriwa jumla ya watu 4.8 milioni watakuwa wameambukizwa Amerika pekee kufikia Juni, mwaka huu.

Ripoti hiyo yenye kichwa ‘What Healthcare leaders need to know: Preparing for COVID-19’, iliandaliwa na Profesa James Lawler wa Chuo Kikuu cha Nebraska Medical Centre.

Takwimu hizo zinaenda kinyume na madai ya Rais wa Amerika, Donald Trump ambaye ameshikilia kuwa hatari ya ugonjwa huo kwa Amerika ni “ndogo”.

Ripoti hiyo ambayo ilipatikana na jarida la “Business Insider” inashauri kuwa, hospitali zinahitaji kuimarisha mikakati ya kupunguza vifo kutokana na maradhi hayo nchini Amerika.

Kufikia Jumamosi, jumla ya watu 17 walikuwa wamethibitishwa kufariki kutokana na virusi vya Corona nchini Amerika huku visa vya maambukizi vikigonga 700.

Kulingana na gazeti la mtandaoni la Daily Mail, watu 96 milioni wataambukizwa maradhi hayo Amerika.

Hii inamaanisha kuwa huenda idadi ya watu waliouawa na kuambukizwa maradhi hayo China yalikoanzia ni kubwa kuliko inavyoripotiwa.

Mnamo Ijumaa, serikali ya Kenya ilipiga marufuku mikutano ya kimataifa nchini na kufungua kituo cha kutenga wagonjwa katika hospitali ya Mbagathi.

Vituo vingine vitafunguliwa katika hospitali za umma katika kila kaunti.

Kufikia Jumamosi, jumla ya watu 3,522 walikuwa wamefariki kutokana na ugonjwa huo duniani, 3,070 wakiwa wamefariki China ambako virusi vya Corona viliripotiwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa 2019.

Na jumla ya watu 103,749 wameambukizwa virusi vya Corona, 80,651 kati yao wakiwa nchini China. Vifo 28 vipya viliripotiwa nchini humo Ijumaa.

Italia, ambako jumla ya watu 197 wamefariki huku visa 4,636 vikiripotiwa ndilo taifa ambalo limeathirika zaidi na ugonjwa huo nje ya China.

Linafuatwa na Iran ambako watu 145 wamefariki huku 5,823 wakiambukizwa. Na nchini Korea Kusini, watu 48 wamefariki huku walioambukizwa wakifikia 7,041.

Katika bara la Afrika, Misri imethibitisha visa 15 vya maambukizi, Senegal (4), Cameroon (2), Morocco (2) huku kisa kimoja kikithibitishwa katika mataifa ya Tunisia, Afrika Kusini na Togo, mtawalia.

Ripoti hiyo ya Profesa Lawler pia inafichua kuwa, watu wenye umri mkubwa wako katika hatari kubwa ya kufariki kutokana na virusi vya Corona kuliko wale wenye umri mdogo.

“Watu wenye umri wa zaidi ya miaka 80 wana kiwango cha asilimia 14.8 ya kufariki wakiambukizwa,” inasema.

Uwezekano wa vijana kufariki kutokana na virusi hivyo ni mdogo, ilhali watu wenye umri kati ya miaka 70 na 79 na 60 na 69 wanakabiliwa na hatari ya kufariki kutokana na virusi vya Corona kwa kiwango cha asilimia 8 na 3.6, mtawalia.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, kuna hatari ya maradhi hayo kusababisha hasara kubwa ulimwenguni.