HabariSiasa

Handisheki bila matunda

March 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MUAFAKA wa maelewano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, maarufu kama handisheki haujazalisha matunda mengi mbali na kuleta hali ya utulivu wa kisiasa nchini unapoingia miaka miwili Jumatatu hii.

Ingawa lengo lao lilikuwa kuunganisha nchi na kuweka mandhari bora ya kukuza uchumi na kufanikisha utekelezaji wa Ajenda Nne za maendeleo, wadadisi wasema mipango mingi imekwama au kuvurugwa, huku ikisalia miaka miwili pekee kabla Uchaguzi Mkuu uandaliwe.

Wadadisi wanasema kwamba, handisheki imezua uhasama mkuu kinyume ya matarajio, hasa kwa kuonekana kumtenga kisiasa Naibu Rais William Ruto.

“Handisheki imeleta mgawanyiko wa kisiasa nchini. Rais Kenyatta na Bw Odinga wanaonekana kumtenga Dkt Ruto, ambapo hiyo ndiyo sababu kuu inamfanya aendelee kulalamika,” akasema Bw Andati  kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa, lengo kuu la Bw Odinga limekuwa kutumia handisheki na Mpango wa Maridhiano (BBI) kuendeleza azma yake ya kuwania urais mnamo 2022.

“Lengo la kwanza la handisheki lilikuwa zuri. Hata hivyo ujio wa Bw Odinga umeisambaratisha Jubilee. Ni kama sasa yuko serikalini, huku Dkt Ruto akibaki nje,” akasema Bw Andati.

Dalili za mgawanyiko Jubilee zilifika kileleni Jumamosi Dkt Ruto alipodai kuna watu serikalini wanafanya kila juhudi kumzima asiwe rais ifikapo 2022.

Wadadisi pia wanasema mpango huo umeondoa uwajibikaji serikalini, kwani hakuna kiongozi shupavu wa upinzani.

“Bw Odinga alikuwa kiongozi wa muungano wa NASA. Alikuwa akiikosoa serikali. Hakuna upinzani kwa sasa. Mashirika ya kijamii pia yamenyamazishwa,” akasema Bw Andati.

Mpango huo pia ulilaumiwa kuchangia mipango muhimu kama Ajenda Nne Kuu za Maendeleo kusambaratika.

Alipoanza muhula wake wa pili mnamo 2017, Rais Kenyatta aliorodhesha uzalishaji vyakula cha kutosha, ujenzi wa nyumba za bei nafuu, afya kwa wote na utengenezaji bidhaa kama masuala ambayo angeyapa kipaumbele katika serikali yake.

Lakini ikiwa imesalia chini ya miaka miwili ili kukamilisha muhula wake, miradi mingi chini ya mipango hiyo imekwama.

Mnamo Januari, Serikali ilipokea nyumba 228, ambazo ni sehemu ya nyumba 500,000 ambazo inalenga kukamilisha kujenga ifikiapo 2022.

Na licha ya taswishi ambazo zimekuwepo, Katibu katika Wizara ya Ujenzi Bw Charles Hinga anasisitiza kwamba serikali inajizatiti kufanikisha mpango huo.

Changamoto kama hii pia inaandama mpango wa uzalishaji chakula cha kutosha, hasa baada ya kubainika kuwa karibu Wakenya milioni kumi hawana chakula cha kutosha. Takwimu hizo zilitolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kenya (KARI).

Kuhusu mpango wa afya kwa wote uliozinduliwa mnamo 2018, wadadisi wameeleza wasiwasi ikiwa utafaulu.

Baadhi ya vikwazo vinavyoonekana kuukumba mpango huo ni mabadiliko yaliyotangazwa majuzi na Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Hospitali (NHIF), kwamba kadi moja haiwezi kugharamia matibabu ya mtu aliye na zaidi ya mke mmoja.

Rais Kenyatta alilazimika kusimamisha mipango hiyo kwa muda baada ya malalamishi mengi kutoka kwa Wakenya.

Na kutokana na hayo, Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuwa, huu ni wakati muhimu kwa Rais Kenyatta kutathmini nafasi ya handisheni, ili kuhakikisha haizamishi malengo na ahadi alizotoa kwa Wakenya.