Habari

Twiga wa kike mweupe wa pekee nchini Kenya auawa na wawindaji haramu

March 10th, 2020 1 min read

Na KENNEDY KIMANTHI

WAWINDAJI haramu wamuua twiga wa kike na mweupe wa pekee Kenya pamoja na mtoto wake, amesema Meneja wa hifadhi ya Ishaqbini Hirola, Bw Mohammed Ahmednoor.

Bw Ahmednoor amesema vifo vya twiga hao vimethibitishwa na walinzi wa hifadhi na jamii pana hapo katika Kaunti ya Garissa.

Mizoga ilipatikana ikiwa imebaki mifupa tupu, kumaanisha walikufa kitambo.

“Ni habari za kusikitisha hasa kwa jamii ya Ijara na Kenya kwa jumla kwa sababu imekuwa fahari kwetu kujivunia twiga mweupe duniani. Ni hamasisho tuamke ili kupambana na uwindaji haramu,” amesema Bw Ahmednoor.

Twiga huyo aligonga vichwa vya vyombo vya habari mwaka  2017 baada ya kugundulika, hasa kichwa chake cheupe. Ni mweupe lakini sio albino kwa sababu ya hali inayoitwa ‘leucism’ ambayo husaidia mnyama kutoa chembechembe nyeusi na ndiyo maana macho yake yalikuwa na weusi.

“Ni pigo kubwa kwa sababu twiga mweupe amekuwa kivutio cha watalii nchini Kenya,” ameongeza.

Agosti 2019, Wakfu wa Northern Rangelands (NRT) ulitangaza kwamba twiga wa kike alikuwa amezaa katika hifadhi hiyo ya Ishaqbini Hirola.

Kuzaliwa kwa ndama wa kiume kuliifanya idadi kuwa watatu twiga wote weupe wanaofahamika.

“Baada ya mkasa huu, ni twiga wa kiume mkomavu mmoja tu anayesalia,” amesema Bw Ahmednoor.