Habari

Corona yatisha kuliko ugaidi

March 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

VALENTINE OBARA na MASHIRIKA

HATUA zinazoendelea kuchukuliwa kimataifa kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona, zinathibitisha jinsi ugonjwa huo ulivyo hatari kuliko majanga mengine mengi yanayokumba dunia, ikiwemo ugaidi.

Ijapokuwa ni wagonjwa takriban asilimia tatu pekee waliofariki kutokana na homa hiyo kufikia sasa, hatari iliyopo ni jinsi inavyovuka mipaka ikienea kwa kasi kimataifa ilhali hakuna tiba wala chanjo iliyopatikana kufikia sasa.

Uchumi pia unadorora ulimwenguni kwa sababu ya ugonjwa huo.

Watu zaidi ya 116,000 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa kufikia jana na zaidi ya 4,000 kati yao kufariki..

Viongozi na wadau wa masuala ya matibabu ulimwenguni wanahimiza watu kukumbatia kila mbinu inayowezekana kuzuia maambukizi, hali ambayo inabadilisha hali ya maisha ya kila siku.

Katika mataifa mengi, ikiwemo yale ambayo bado hayajapokea mgonjwa yeyote wa virusi vya corona, hali ya maisha inabadilika nyumbani, kazini na katika maeneo ya kukongamana kama vile makanisani.

Salamu za mikono zinaepukwa, sawa na mabusu na pambaja. Badala yake, kuna watu wanaosalimiana kwa kugongana viatu miguuni, kukodoleana macho au kupungiana mikono kutoka mbali.

Jijini Beijing, China, jiji kuu la taifa ambapo coronavirus ilianzia, mabango mekundu yamewekwa barabarani kushauri watu wasisalimiane kwa mikono. Badala yake wanashauriwa wajishike mikono yao wenyewe kuashiria salamu kwa wenzao. Kuna pia vipaza sauti ambavyo vinakumbusha watu kwamba wanaweza ‘kugoteana’ badala ya salamu za kawaida walizozoea.

Mbinu ya salamu za kukodoleana macho nayo inashuhudiwa sana Ufaransa ambapo kwa kawaida watu husalimiana kwa mabusu.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Usalama wa Ujerumani Horst Seehofer alikataa salamu za mkono kutoka kwa Waziri Mkuu Angela Merkel.

Ibada makanisani pia zimeathirika. Nchini Italia, makanisa mengi hayakufunguliwa wikendi iliyopita.

Nchini Poland, waumini wamelazimika kubadili mbinu za kula sakramenti. Wamezuiliwa pia kuingiza mikono yao ndani ya maji matakatifu wanapoingia au kuondoka kanisani na badala yake wanahitajika tu kufanya ishara ya msalaba.

Huku Sikukuu ya Pasaka ikikaribia, mataifa yaliyo na idadi kubwa ya Wakristo hasa waumini wa Kanisa Katoliki, yanatarajiwa kuwa na changamoto zaidi.

Mfano ni Uhispania ambapo kwa kawaida Wakatoliki hupiga busu sanamu za Bikira Maria wiki moja kabla ya kusherehekea Pasaka. Waumini hujitokeza kupiga busu mikono au miguu ya sanamu za Maria na za watakatifu wengine wakiomba baraka maishani.

Afisa katika idara ya kitaifa ya afya nchini humo, Fernando Simon alisema kuna uwezekano desturi hiyo itapigwa marufuku mwaka huu.

Hali hii imeathiri pia harusi zilizokuwa zimepangwa, kukiwa na ripoti zinazoonyesha wengi wameamua kufutilia mbali sherehe za harusi kwa sasa.

Kukongamana katika maeneo ya burudani ikiwemo vilabuni na viwanja vya michezo pia haiwezekani katika nchi zilizoathirika zaidi.

Endapo kuna maeneo yanayofunguliwa, waliomo huhitajika kukaa angalau futi tatu kutoka kwa wenzao.

Raia wa Brazil walipata pigo kwani mazoea yao ya kunywa kahawa kwenye jungu moja na wenzao wakitumia mirija sasa ni marufuku.

Katika michezo, Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte mnamo Jumatatu alisimamisha mashindano yote ya michezo nchini humo hadi Aprili 3.

“Hakuna haja kuruhusu mechi na mashindano mengine ya michezo kuendelea…lazima mashabiki wazingatie hali ilivyo. Hatutaruhusu michezo katika ukumbi wowote,” akaeleza.

Elimu pia imekwama. Mamilioni ya wanafunzi wa shule na taasisi za elimu ya juu wameagizwa kukaa nyumbani kwa muda usiojulikana katika nchi zilizo na idadi kubwa ya maambukizi ya coronavirus.

Ijapokuwa hakuna maambukizi yametangazwa Kenya, Chuo cha Catholic University of Eastern Africa (CUEA) tayari kimeagiza wahadhiri waandae mifumo ya kutoa mafunzo kupitia intaneti kabla Machi 20.

Imebainika pia kuna kampuni kadhaa ambazo zinafanya maandalizi kuhusu jinsi wafanyakazi watatoa huduma bila kwenda ofisini iwapo maradhi hayo yatazuka Kenya.

Wafanyakazi kadhaa nchini China, Amerika, Japan na Italia waliagizwa kutoenda kazini na badala yake wanafanya kazi zao kupitia intaneti wakiwa nyumbani. Mfano kampuni ya Twitter na Apple.

Kando na kutumiwa kufanya kazi za ofisini kutoka nyumbani, teknolojia pia inatumiwa zaidi sasa katika mataifa yanayokumbwa na mkurupuko huo kufanya mahojiano bila kukutana na mtu kibinafsi, kuendesha ibada kimitandao, uagizaji bidhaa ikiwemo vyakula na burudani.

“Tunaweza kuletewa chochote na hata kila kitu nyumbani kwetu, ikiwemo kupokea ushauri wa daktari aliyehitimu kupitia kwa mitandao,” akasema mchanganuzi katika kampuni ya Moor Insights Patrick Moorhead.

Huenda kikundi cha watu wanaoweza kusemekana wamebahatika na mkurupuko huu ni wafungwa nchini Iran ambapo watu 43 wamefariki kutokana na virusi vya corona. Serikali iliamua kuwaachilia huru wafungwa takriban 70,000.