• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
KINA CHA FIKIRA: Malimbukeni wa tafsiri wasioomba kukwamuliwa ni hatari kwa tasnia hiyo

KINA CHA FIKIRA: Malimbukeni wa tafsiri wasioomba kukwamuliwa ni hatari kwa tasnia hiyo

Na KEN WALIBORA

SIKU hizi ukiona mtu akiuliza kisawe cha Kiswahili cha neno na usemi wa Kiingereza basi yamkini amepata kazi ya kutafsiri.

Hawezi kukuambia kama keshapata hiyo kazi. Atakurushia tu swali au kwa kundi la watu kisha arudi chumbani kumenyana na kazi yake kimyakimya kama kobe katika ganda lake. Na maswali kama haya yanaibuka kwenye majukwaa ya kama vile Facebook, WhatsApp, Twitter au kwa ujumbe mfupi wa simu.

Kwa hiyo, unaona maswali kama neno “compromise” au “reptile,” nini kisawe chake katika Kiswahili? Unakaa unashangaa kwa nini mtu anasumbuka na visawe vya maneno haya, kumbe ni kutanzwa na kazi ya tafsiri “iliyomwangukia.”

Hili linadhihirisha kwamba kwa kweli kazi za tafsiri zipo. Huwa zinatokeatokea kama uyoga hapa na pale, na wale wanaotembea vizuri huziangukia, au huwa zinawaangukia. Natumia neno “kuangukia” hapa kama linavyotumiwa na baadhi ya watu siku hizi. Mpwa wangu alimwambia mdogo wake hivi karibuni, “kaka kwa hakika umeangukia mke mzuri.” Nafikiri alichomaanisha ni kwamba mkubwa wake kapata bahati ya kumwoa mke bulibuli wa kupendekeza, labda kwa uzuri na tabia. Lakini huku “kuangukia” kunabeba maana nyingine kwamba mambo yanakwenda kwa nasibu, kwa bahati. Unakuwa wewe mja wa Mungu pale ulipo huna satua, ni nasibu tu ndiyo inayoamua kama unapata au unakosa. Yamkini mchakato wa kupata kazi ya tafsiri unakwenda hivyo humu nchini, huwa watu wanaangukiwa tu au inawaangukia tu tafsiri kama mpwa wangu alivyoangukia mke mzuri.

Kwa hiyo watafsiri wetu wasiokuwa na umilisi na kujiamini wameketi walipoketi, wanasubiri bahati ya kutafsiri iwaangukie, au waiangukie kazi ya tafsiri waanze kufanya tafsiri. Waiangukie au iwaangukie kazi ya tafsiri ya matangazo ya biashara, makala, makabrasha, vijitabu, na vitabu.

Wakishapata tu, basi wanaanza kutapatapa na kukera watu kwa maswali hebu nipe kisawe cha “compromise” na “reptile” kwa Kiswahili.

Wanapoanza kuuliza tu, unajua kwamba wamekwama wanahitaji kukwamuliwa ila hawasemi wamekwama katika tafsiri. Utafikiri ni watu wanaotafuta tu kutanua upeo wa msamiati wao wa Kiswahili. Kumbe ni riziki inasuasua. Tafsiri imekwama, mbele haiendi na nyuma hairudi. Mtu kaaminishwa kumbe haaminiki. Naam, kaaminishwa kutafsiri kumbe unga umezidi maji au maji yamezidi maji.

Lakini wanafanya jambo zuri: wanauliza na wasemao husema, “kuuliza si ujinga.” Wapo wengine wanaopuuza kabisa hekima ya methali hii. Hawaulizi chochote. Wanakwenda tu kiupofu upofu, si laiki yao kuuliza. Hawa ndio wanaokuandikia Corona Virus kwenye taarifa za Kiswahili, hawataki kuuliza kama ni sawa au si sawa kutoliswahilisha neno la asili kwengine. Hawajui ukitaka kuswahilisha “C” ya maradhi haya hatari, itabidi ibadilike iwe “K” na virusi kuwa kirusi. Hawajui twasema ama kirusi cha korona au ugonjwa wa korona. Ila hawa hawasemezeki hawaambiliki. Hawa ndio maadui wakubwa wa Kiswahili kuliko malimbukeni wanaomba kukwamuliwa bila kufichua wana kazi ya tafsiri.

You can share this post!

WASIA: Yadumishe macho na akili yako kwenye mustakabali wako

KAULI YA MATUNDURA: Mazingira ya kisiasa na kiuchumi katika...

adminleo