Habari

Kenya ni ngome ya uhalifu mitandaoni na wizi wa hakimiliki barani Afrika – utafiti

March 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KENYA ni mojawapo ya ngome kuu barani Afrika katika uhalifu mitandaoni na wizi wa hakimiliki, utafiti mpya umeonyesha.

Utafiti huo pia umedhihirisha kwamba, japo idadi kubwa ya Wakenya wanajihusisha na uhalifu huo, raia wa kawaida hawafahamu kuhusu madhara ya vitendo vyao.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi mnamo Jumanne, Mkurugenzi wa Bodi ya Hakimiliki Nchini (Kecobo) Edward Sigei amesema pana haja ya kuwahamasisha Wakenya dhidi ya kujihusisha na wizi wa hakimiliki na utumiaji bila idhini wa makala na matini kwa jumla kwa lengo la kukomesha uhalifu huo nchini.

“Ripoti za hivi majuzi na data iliyokusanywa kuhusu uhalifu mitandaoni ikiwemo wizi wa haki miliki imeorodhesha Kenya kama kituo kikuu. Kwa bahati mbaya, Mkenya wa kawaida hafahamu kuhusu madhara yasiyo ya kimaksudi ya vitendo na shughuli zao zinazohusu wizi wa hakimiliki,” ameeleza Bw Sigei.

Akionekana kuunga mkono kauli ya Mkurugenzi huyo, Mwenyekiti wa Muungano wa Wachapishaji Kiarie Kamau amesema: “Kuna upigaji chapa mwingi unaofanyika katika vyuo vikuu lakini hawajui ni makosa kwa kuwa wanaua ubunifu. Uhamasishaji unahitajika huku utekelezaji sheria ukifanyika.”

Kulingana na utafiti uliofanywa majuzi na Irdeto, shirika la kimataifa kuhusu usalama mitandaoni, wizi wa hakimiliki za matini hugharimu serikali, sekta za michezo na ubunifu kiasi cha Sh5125 trilioni kote ulimwenguni.

Isitoshe, ripoti hiyo imefichua kuwa, maendeleo katika teknolojia na utandawazi yamechangia pakubwa kuendeleza wizi wa hakimiliki kwa kuwarahisishia wahalifu kupata matini huku uchumi na tamaduni kote duniani zikiunganishwa na kuingiliana.

Kuonyesha filamu na kucheza muziki kinyume na sheria, pataning DVD, vifaa vya kuhifadhia matini vilivyo ghushi, vifaa bandia vya kusambazia ishara ni baadhi ya mitindo inayotumiwa kuendeleza uhalifu huo wa wizi wa hakimiliki barani Afrika na kote ulimwenguni kulingana na utafiti huo.

Katika juhudi za kukomesha uhalifu huo nchini na kutoa uhamasishaji, Kecobo imezindua kampeni kwa jina Washiriki Dhidi ya Wizi wa Hakimiliki (APA).

“Kampeni hii itasaidia umma kutofautisha baina ya bidhaa halisi na zile bandia huku ikiwapa changamoto kusita kabla ya kufanya uamuzi wa kununua kwa kuzingatia athari na manufaa ya ununuzi huo,” amefafanua Bw Sigei.

Kuhusu suala la kujumuisha teknolojia katika kukomesha uhalifu huo, mkuu wa Kecobo ameeleza kuwa mchakato unaendelea wa kupata vifaa vya kisasa vya kuwatambua, kuwafuatilia na kuwanasa wezi wa hakimiliki kufuatia amri ya Rais Uhuru Kenyatta.

“Rais aliipa afisi yangu makataa ya miaka mitano baina ya 2017-2022 kuhakikisha ina vifaa vya kisasa vinavyoweza kutumika kuwanasa wanaoendeleza uhalifu huo,” ameeleza.

Mnamo Septemba 2019 Kiongozi wa Taifa alitia sahihi kuwa sheria, Mswada Uliofanyiwa Marekebisho kuhusu Wizi wa Hakimiliki (2019), hatua ambayo iliipa Kecobo mamlaka zaidi kuangazia na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wezi wa hakimiliki nchini.