COVID-19: NOC-K yataka mashirikisho yasitishe michezo
Na GEOFFREY ANENE
KAMATI ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (NOC-K) imetaka mashirikisho yote ya michezo nchini yasimamishe michezo ya umma jinsi serikali imeagiza ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi hatari vya corona.
Wizara ya Afya ilitangaza Ijumaa kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi hivyo, ambavyo vinahangaisha dunia nzima.
“Kamati ya NOC-K inaomba mashirikisho wanachama kusimamisha shughuli zao za michezo jinsi serikali imetangaza na kutilia maanani maagizo ya Wizara ya Afya yanayogusia masuala mengi yakiwemo usafiri, usafi wa mtu binafsi na kuandaliwa kwa shughuli za umma.
“Ingawa mashindano mengi ya kuchagua timu za Olimpiki 2020 yamesimamishwa kwa sababu ya mkurupuko wa virusi hivyo, NOC-K inawasiliana na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) mara kwa mara kuhakikisha wanaspoti wanapata haki sawa ya kushiriki makala ya Olimpiki ya mwaka huu,” NOC-K imesema.
Mashindano ya judo na miereka ya kufuzu kushiriki Olimpiki 2020 yalifutiliwa mbali. Timu za Kenya za voliboli ya ufukweni za wanaume na wanawake zilishindwa kusafiri hadi nchini Gambia na Nigeria kwa sababu sawa na hizo.
Wakenya wanaoshiriki mchezo wa upigaji wa makasia ni wa hivi punde kuathiriwa. Timu hiyo ilirejea nchini Alhamisi kutoka nchini Ufaransa ilikokuwa imefika mjini Hinningue kabla ya mashindano hayo kufutiliwa mbali.
“Haya yakijiri ni muhimu kufahamu kuwa NOC-K imejitolea kwa dhati kuendelea kuandaa timu ya Kenya kwa mashindano ya Tokyo 2020. Tungependa kutia moyo wanamichezo wetu kuwa waendelee na mazoezi yao ya kibinafsi, kwa sababu usalama wa kila mchezaji ni muhimu sana kwetu,” kamati hiyo imesema.