Kivumbi cha kumrithi Joho chatifuka, Mboko yumo pia
Na WINNIE ATIENO
SIASA za kumrithi Gavana Hassan Joho zimepamba moto huku wabunge wakijizatiti kupata ‘baraka’ za kinara huyo wa Kaunti ya Mombasa.
Wabunge Bi Mishi Mboko (Likoni), Bw Abdulswamad Nassir (Mvita), Bw Ali Mbogo (Kisauni), Bw Badi Twalib (Jomvu), Bw Omar Mwinyi (Changamwe) na spika wa bunge la Kaunti ya Mombasa Harub Khatri, wako mbioni kusaka umaarufu huku wakisubiri kutawazwa na Bw Joho ambaye ana usemi mkubwa wa siasa za eneo la Pwani.
Bw Joho anachukuliwa kama msemaji wa siasa eneo la Pwani na wanasiasa wengi wamekuwa wakimfuata kupata baraka zake hususan wale wa chama cha ODM.
Hata hivyo, Bw Joho ambaye anamaliza hatamu yake ya ugavana baada ya kuongoza kwa vipindi viwili, amesalia kimya kuhusu suala la mrithi wake.
Bw Joho yuko katika njia-panda kwani wandani wake wanatarajia awatawaze kumrithi.
Bi Mboko alisema anamsubiri gavana huyo kuamua mrithi wake.
“Tuache kujipiga vifua, kupiga kelele na kuringa eti ooh sijui nini na nini, Bw Joho atasawazisha kila kitu, yeye ndiye atakaye amua. Lakini kama wanawake, ninawasihi tuanze kujipanga mapema ili tupate kura nyingi zaidi,” alisema Bi Mboko.
Alisema wabunge wote wanaotaka kumrithi gavana huyo ni wanafunzi wake wa kisiasa.
“Bw Nassir na mimi tunataka ugavana na sote tuko upande wa gavana wetu, kwa hivyo wacheni propaganda za kugonganisha watu. Bw Mwinyi, Bw Mbogo, Bw Khatri na mimi Mishi Mboko sote tunavizia kiti cha ugavana,” alisema.
Bi Mboko ni mwanamke wa kwanza kugombea ugavana wa Mombasa ambayo ina wapiga kura 500,000.
Alisema ananuia kuwaunganisha wanawake na vijana ili kupata kura zao. Awali alitajwa kuwa mbichi katika siasa za Mombasa, lakini katika siku za hivi majuzi amejitokeza kama mwanasiasa shupavu akimenyana na wanaume.
Akiongea kwenye sherehe za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mnamo Machi 3 Bi Mboko alisema yuko tayari kumrithi Bw Joho kwani ana kisomo na amekomaa kwenye siasa.
Alisema licha ya kupakwa tope, amejizatiti kwenye ulingo huo baada ya kumenyana na wanaume kwenye uchaguzi wa ubunge wa Likoni mwaka wa 2017.
Bi Mboko mwenye shahada ya Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Moi, aliandikisha historia baada ya kuwa mwanamke wa kwanza Mombasa kuchaguliwa mbunge.
Hata hivyo, mwanachama huyo shupavu wa ODM alikisihi chama chake kuhakikisha usawa katika ugavi wa uongozi mwaka wa 2022.
“Yeyote anayegombea kiti cha ugavana anafaa kutathminiwa kulingana na maendeleo aliyoyatekeleza akiwa mbunge. Lakini tusiwe na mori, uongozi wa ODM utakaa chini na kuamua atakayemrithi Bw Joho,” alisisitiza.
Bw Mbogo alichagulia kupitia tikiti cha Wiper huku Bw Twalib, Bw Mwinyi na Bw Nassir ni wa chama cha ODM.
“Ninampenda sana Bw Joho, ni shupavu, mweledi na wala haogopi mtu yeyote. 2022 lazima awakilishe Pwani katika serikali kuu, lazima tumsikilize na tuyafuate maneno yake ili tufaidike sababu ni kiongozi wetu,” alisema Bi Mboko akisisitiza akuwa wanawake wa pwani hawatoachwa nyuma uongozini.
Alisema Bw Joho, gavana wa Kilifi Amason Kingi na kiongozi wa ODM Raila Odinga walimsaidia na kufanikisha malengo yake kwenye siasa.
“Mimi na Bi Aisha Juma hatukupitia mchujo, tulipewa tikiti moja kwa moja tukiwa nyumbani mwake nduguye Bw Joho, Bw Abu huko Nyali. Niliwaambia niko tayari kumenyana na wanaume na wakanipa baraza zao hivyo ndiyo mimi na Bi Jumwa tulivyowafungulia nafasi wanawake wengine kuingia bungeni,” alisisitiza.
Naye mwakilishi wa wanawake wa Mombasa Bi Aisha Hussein alionya wanasiasa dhidi ya kupaka tope viongozi wanawake.
“Omba kura pole pole wacha kupaka wanawake matope. Na kama wewe ni mwanamke mwenzetu, tushikane,” alisema.
Lakini mchanguzi wa maswala ya kisiasa Bi Grace Oloo alisema Bi Mboko hana nafasi ya kumrithi Bw Joho.
“Kwanza kabisa taasubi ya kiume huku pwani bado ni ile ya jadi, hawawezi kumpa mwanamke kura, pili ni maendeleo gani ameleta Likoni?” aliuliza.
Bi Oloo alisema wanawake wana safari ndefu kabla ya kupata ugavana wa Mombasa.