Makala

AKILIMALI: Alitambua kipaji chake katika ususi akiwa shuleni

March 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kuhitimisha elimu ya sekondari kwa kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE mnamo 2013, matamanio ya Faith Kanini yalikuwa kusomea kozi inayohusiana na masuala ya ususi na urembo ‘Hair dressing & beauty therapy’.

Ni sanaa inayohusisha macho, akili na mikono. Faith anasema akiwa katika shule ya msingi na upili, alisuka wanafunzi wenza, hivyo basi alianza kujitayarisha na kunoa bongo akiwa angali mdogo kiumri.

Akiwa mzaliwa wa eneo la Munyu, kaunti ndogo ya Thika, 2014 alihamia Nairobi alikoishi na shangazi yake ili kusomea ususi. “Nilijisajili katika chuo kimoja cha ususi na urembo jijini Nairobi, nikaanza mafunzo,” Faith anasema.

Kozi hiyo aliisomea kwa muda wa miezi sita mfululizo, na ikizingatiwa kuwa alikuwa na uzoefu, anasema kufikia mwezi wa tatu wa mafunzo alikuwa amebobea.

“Nilianza kupata vibarua nikiwa chuoni. Nilipokamilisha mafunzo nilikuwa nimepata mtaji wa kuanzisha duka langu binafsi (saluni),” Faith, 23, aelezea. Hata ingawa hakuanzisha kwa mashine za hadhi ya juu, anafichua kwamba alitumia mtaji wa Sh30, 000 kung’oa nanga.

Muhimu zaidi kulingana naye ni mmoja awe anaelewa bayana namna ya kusuka nywele. Aidha, kuna mashine za kulainisha nywele kama vile ‘blow dry’ miongoni mwa zingine.

Faith anasema alitangulia kwa kulenga eneo bora, lenye idadi kubwa ya watu, akichagua mtaa wa Mwiki, ulioko Kaunti ya Nairobi. “Japo nilikuwa na wateja walionitegemea, nilitafuta eneo litakaloniboresha,” asema, akiongeza kusema kuwa mikakati aliyoweka ilifanikishwa kwa kuandaa mwongozo wa biashara.

Anafafanua kuwa, hatua hiyo pia ilijumuisha kujua vigezo muhimu kuanzisha duka la ususi na urembo, ikiwamo mahitaji kisheria kama vile leseni ya biashara.

“Kupitia mwongozo huo na utafiti wa kina, nimefanikisha kutoa huduma za kipekee,” asema.

Samuel Karanja, ambaye ni gwiji katika masuala ya ususi anasema vigezo vingine muhimu kuzingatia katika sanaa hiyo ni kujua wauzaji wa malighafi ya ususi na urembo kwa kijumla, wanaouza bidhaa hizo kwa bei nafuu. Anasema hatua hiyo inasaidia kupunguza gharama kwa kiasi kikuu.

“Ukiwa na wafanyakazi, jali maslahi yao. Hakikisha mazingira yao ya kazi ni bora na ya kuridhisha, bila kusahau malipo bora ikiwa wanakuingizia mapato,” Karanja anaeleza.

Katika mukhtadha huo, Faith Kanini ambaye pia ni mama wa watoto wawili anasisitiza kuwa wateja amewapa kipau mbele. Huduma anazotoa zinaenda sambamba na matakwa yao.

“Malipo ya staili na miundo ya ususi na huduma zingine ni ya bei nafuu,” aeleza, akidokeza kwamba ada anayotoza ni kati ya Sh100 hadi Sh5,000.

Aidha, husuka miundo na staili kama vile; Pencil braids, Twisting, Bridal – Maids Hair Style na Make up.

Miundo mingine ni Ghanaians, Weaving, Closer na Box/Bob braids.

Mbali na miundo ya nywele, huduma za urembo anazotoa ni kusafisha, kung’arisha kucha na kuzipaka hina, manicure na pedicure.

Faith ana mfanyakazi mmoja, na kando na kuendelea kuboresha talanta yake, anasema anapania kufungua chuo cha kutoa mafunzo.

Stadi Samuel Karanja ana maduka kadha ya saluni Nairobi na pia ana chuo cha mafunzo ya ususi na urembo eneo la Githunguri, ambacho alikifungua miaka miwili iliyopita. Mwaka uliopita, kundi la kwanza la wanafunzi lilifuzu kwa vyeti na stashahada.

“Kwa walio kwenye sanaa hii, kila kitu kinawezekana kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Nilianza kama msusi tamba, nikafungua saluni kadhaa Nairobi kisha chuo cha mafunzo. Cha msingi ni kutia shime na bidii kazini,” ashauri.

Sawa na barobaro huyo, Faith pia anahimiza vijana kutolaza damu, “ninawahimiza wapalilie talanta na vipaji vyao badala ya kutegemea gange za ofisi na ambazo ni haba mno nchini”.