• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
FKF Nairobi Magharibi yapata viongozi wapya

FKF Nairobi Magharibi yapata viongozi wapya

Na JOHN KIMWERE

LICHA ya mkurupuko wa virusi hatari vya Corona hapa nchini uchaguzi wa Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF) katika Kaunti zote tisa uliendelea kwa amani. Uchaguzi huo uliandaliwa katika Kaunti za Nairobi, Nyamira, Nyeri, Turkana, Trans Nzoia, Kisii, Kisumu, Garissa na Kwale.

Katika Kaunti ya Nairobi Tawi la Nairobi Magharibi, kundi la aliyekuwa katibu wa tawi hilo, Caleb Ayodi Malweyi lilitwaa nafasi zote tano na kuahidi kushirikiana na waliokuwa wapinzani wao kusaidia soka eneo hilo.

Caleb Ayodi Malweyi alichaguliwa mwenyekiti mpya baada ya kumshinda Charles Ng’ang’a Njoroge na mgombea mwenza, Fredrick Okoth Amolo. Malweyi aliwania wadhifa huo na mgombea mwenza wake, Alfred Mutua Muli ambapo alipata kura 44 dhidi ya 17.

”Kwanza nashukuru wote kwa kuonyesha wana imani nami kuongoza tawi la Nairobi Magharibi kwenye juhudi za kukuza soka ndani ya miaka minne ijayo,” Caleb alisema baada ya kutangazwa mshindi.

Aidha alisema alipofikia uamuzi huo aliongea na aliyekuwa mwenyekiti wake maana katika uongozi wa soka hawastahili kuwa maadui.

Katika wadhifa wa katibu, Charles Kioko Kaindi alizoa kura 55 dhidi ya sita za mpinzani wake, Martin Karanja. Nao Maureen Obonyo na Josphat Karuri walihifadhi nyadhifa zao kama mwakilishi wa wanawake na mweka hazina mtawalia.

Wadhifa wa Mwakilishi wa vijana ulimwendea Hannington Khayati aliyekusanya kura 46 naye Moses Oduor Were alipata 15. Maureen Obonyo aliibuka mshindi kwa kupata kura 49 dhidi ya kura 12 zake Susan Nyanganyi Mudongoi.

”Tunapania kuweka mikakati kabambe kuhakikisha tunakuza talanta za wachezaji chipukizi wavulana kwa wasichana katika matawi yote,” alisema Hannington Khayati na kuongeza kuwa aliyeshikilia wadhifa huo kipindi kilichopita hakufanya kazi ilivyotarajiwa.

Khayati alisema kuwa tayari tumejadiliana na maofisa wenzake kuhusu hatua ya kuanzisha ligi za mchezo huo kwa wachezaji wanaokuja eneo hilo ili kuhakikisha kuwa chini ya kipindi cha miaka minne ijayo wamekuza talanta kadhaa.

NYAMIRA

Katika Tawi la Nyamira, wadhifa wa mwenyekiti mpya ulimwendea Luthers Mokua aliyezoa kura 14 naye mpinzani wake alipata kura sita.

Katibu alichaguliwa Vincent Nyasani kwa kupata kura 14 huku Evans Onderi alipigiwa kura sita. Naye David Kireki alitangazwa mweka hazina kwa kuzoa kura 13 mpinzani wake, Emmaculate Onkangi alizoa kura saba.

KWALE

Katika tawi la Kwale, Hamisi Mwakoja alichaguliwa mwenyekiti mpya kwa kuzoa kura tano dhidi ya mbili zake mpinzani wake Salim Bambaulo. Bakari Hamisi Zamu alipigiwa kura tano na kutangazwa mweka hazina mpya alipomshinda Juma Mwalivundo aliyezoa kura mbili.

You can share this post!

CORONA: Hofu yatanda Baringo

CORONA: Utalii kuathirika zaidi

adminleo