Habari

CORONA: Maisha ya Wakenya yabadilika

March 17th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MAISHA ya Wakenya yamebadilika pakubwa katika muda wa siku nne zilizopita, baada ya virusi vya corona kuambukiza baadhi ya watu nchini.

Kuanzia Ijumaa iliyopita wakati serikali ilipotangaza mgonjwa wa kwanza alipatikana Kenya, wananchi walianza kufuata tabia za wakazi wa mataifa yaliyotangulia kupata maambukizi kama vile China na Italia.

Maisha yalizidi kubadilika jana, siku moja baada ya idadi ya wagonjwa kuongezeka.

Kati ya mambo ambayo yamebadilika ni salamu, shughuli za mazishi na harusi, starehe, jinsi watu wanavyofanya kazi, kunawa mikono mara kwa mara na usafiri.

Kabla ya kisa cha kwanza kutangazwa, Wakenya walikuwa wameanza kubadili mienendo yao kama vile kuosha mikono kila mara na kuacha kusalimiana kwa mikono. Hii ni tangu tahadhari ya corona ilipotangazwa kote duniani.

Jumatatu, kaunti mbalimbali ziliweka masharti makali kuepusha uwezekano wowote wa kueneza virusi vya corona. Hatua hizo zitatatiza kwa kiwango kikubwa maisha ya kawaida ya wananchi.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, wanachama wa Nyumba Kumi walipewa mamlaka ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mkazi yeyote atakayekiuka marufuku ya kupiga busu, kuandaa harusi ama matanga.

Maeneo ya Magharibi ya Kenya hufahamika kwa kuandaa matanga na mazishi yanayokaribia kufanana na karamu kubwa zinazohudhuriwa na halaiki ya watu.

Sawa na Trans Nzoia, Kaunti ya Kakamega pia ilipiga marufuku desturi hiyo na kuagiza mochari zifungwe ili mtu anapofariki azikwe mara moja.

Eneo la Pwani, polisi waliokuwa na silaha walitumwa kwenye fuo za Bahari Hindi kuzuia wananchi na wafanyibiashara kufika huko.

Agizo la serikali kufunga shule zote wakati ambapo baadhi ya wazazi watalazimika kufanyia kazi zao nyumbani pia litasababisha mabadiliko makubwa kimaisha.

Kwa kawaida jijini Nairobi, Jumatatu huwa ni siku iliyo na shughuli nyingi zinazosababisha msongamano wa magari na binadamu barabarani na katikati mwa mji. Lakini jana, barabara kadhaa jijini zilikuwa na shughuli chache kuliko kawaida, ikiaminika wakazi wengi waliamua kutoenda mjini.

Katika magari ya uchukuzi wa umma, abiria waliozoea kufunga madirisha sasa wanavumilia kupigwa upepo mkali usoni wakiamini ukosefu wa hewa safi ndani ya gari ni mandhari bora ya kusambaza virusi vya corona endapo kuna abiria yeyote aliye na ugonjwa huo atakayethubutu kukohoa.

Tofauti na ilivyo desturi ya Wakenya kutembelea jamaa na marafiki waliolazwa hospitalini, sasa itakuwa vigumu kwani wasimamizi wameweka masharti makali kupunguza idadi ya watu wanaoingia katika hospitali kwa wakati mmoja.

Kwa mfano, Hospitali ya Aga Khan University jijini Nairobi ilisema itaruhusu mtu mmoja pekee, ambaye ni jamaa wa karibu wa mgonjwa aliyelazwa kuingia chumbani alikolazwa.

“Jamaa wa mgonjwa ataruhusiwa kukaa katika wodi kwa dakika zisizozidi 30 pekee. Zaidi ya hayo, tunaomba wagonjwa wanaohitaji matibabu katika hospitali na kliniki zetu wasiandamane na watu wengi. Ikiwezekana, wapelekwe na mtu mmoja pekee,” hospitali hiyo ikasema kwenye taarifa.

Katika baadhi ya hoteli za mijini, usafi wa hali ya juu uliwekwa ambapo wateja walikuwa wakioshwa mikono langoni.

Wikendi, ni Wakristo wachache kuliko ilivyo kawaida ambao walikuwa na ujasiri wa kwenda kanisani walikutana na wahudumu wa kuwaosha mikono milangoni kabla waruhusiwe kuingia.

Wakati huo huo, siasa ambazo husheheni katika pembe tofauti za nchi kila wikendi hazikushuhudiwa kwani corona imelazimisha serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara.

Wanasiasa walioenda kanisani, aChama cha ODM kupitia kwa Katibu Mkuu Edwin Sifuna, jana kilithibitisha kitapunguza shughuli zake: “Tunachukua hatua kutimiza masharti ya idara ya afya ya umma kuhusu kudhibiti virusi vya corona hapa Kenya. Kwa msingi huu, tunapunguza shughuli zetu katika afisi kuu na pia mashinani hadi hali itakapodhibitiwa,” akasema.

Hapo jana jioni serikali ilisema kuna watu watatu wanaoonyesha dalili za kuugua virusi vya corona, kando na watatu waliothibitishwa kuugua. Matokeo ya hali yao hayakuwa yametokea.

Msemaji wa serikali, Bw Cyrus Oguna, jana alisema watatu hao ni miongoni mwa 22 ambao walikuwa wametangamana na mgonjwa wa kwanza aliyetangazwa Ijumaa.