CORONA: Ada za M-Pesa zapunguzwa
Na WANDERI KAMAU
WAKENYA wanaotuma Sh1,000 kwenda chini kwa njia ya simu hawatatozwa ada yoyote kwa miezi mitatu ijayo kuanzia leo, baada ya kampuni za Safaricom, Airtel na Telcom kuondoa ada hizo.
Hatua hiyo iliafikiwa Jumatatu baada ya mkutano kati ya maafisa wakuu wa kampuni hizo na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Dkt Patrick Njoroge.
Hatua hiyo pia inafuatia ombi la Rais Kenyatta kwa kampuni zinazotoa huduma za utumaji pesa kwa njia ya simu, kutafuta njia mbadala za kuwapunguzia Wakenya hatari ya kuambukizwa virusi vya corona wanapolipia bidhaa kwa pesa taslimu.
Kwenye taarifa, kampuni ya Safaricom pia iliongeza kiwango ambacho mtu anaweza kutuma ama kutoa kwa njia ya M-Pesa kutoka Sh70,000 kwa siku hadi Sh150,000.
Wakenya vile vile wataweza kuweka hadi Sh300,000 kwa simu kutoka Sh140,000 kwa sasa.
“Hatua hii pia inalenga kuwasaidia wenye biashara ndogo ndogo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni hiyo Michael Joseph.
Mnamo Jumapili, Rais Kenyatta aliziomba kampuni zinazotoa huduma hizo kutathmini upya gharama za kutuma pesa kwa njia ya simu ili kupunguza uwezekano wa kugusa sarafu.
Wakati huo huo, kampuni hiyo ilisema kuwa inashirikiana na serikali kwa kubuni nambari 719, ambayo itawapa Wakenya nafasi ya kupata maelezo yoyote wanayohitaji kuhusiana na virusi vya corona.