Makala

KWA KIFUPI: Usafi mdomoni hupunguza hatari ya kisukari – Utafiti

March 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANDISHI WETU

TANGU jadi wataalamu wa kiafya wamekuwa wakipendekeza umuhimu wa kudumisha usafi wa mdomoni kama mbinu ya kuzuia meno kuoza, maradhi ya ufizi na maambukizi mengine ya mdomoni.

Lakini mbali na hayo, imeibuka kwamba usafi huu una manufaa mengine: kupunguza hatari ya kukumbwa na kisukari.

Utafiti uliochapishwa na Diabetologia, jarida la shirikisho la mataifa ya Ulaya linalohusika na uchunguzi wa maradhi ya kisukari, umeoyesha kwamba kudumisha usafi wa mdomoni kunapunguza hatari ya kukumbwa na kisukari aina ya Type 2.

Watu wanaougua maradhi hayo wana viwango vya juu vya sukari kwani hawana uwezo wa kutosha wa kuzalisha kiwango cha kutosha cha homoni inayofahamika kama insulini inayodhibiti viwango vya sukari kwenye damu.

Watafiti hawa waligundua kwamba kusugua meno mara tatu au zaidi kwa siku kulihusishwa na asilimia nane ya upungufu wa hatari ya kukumbwa na maradhi ya kisukari.

Aidha, kuwepo kwa maradhi ya meno kulihusishwa na ongezeko la asilimia nane la uwezekano wa kukumbwa na maradhi ya kisukari.

Isitoshe, watafiti hao wamefichua kwamba kuwa na mapengo ya meno 15 na zaidi kunaongeza hatari ya kukumbwa na maradhi ya kisukari Type 2 kwa asilimia 21.

Kulingana na watafiti hawa, udadisi huu unathibitisha umuhimu wa kudumisha usafi wa mdomoni.

“Kwa ujumla, huenda kuimarisha usafi wa mdomoni kukapunguza hatari ya kukumbwa na kisukari,” walisema.

Kulingana nao, huenda uhusiano baina ya usafi wa mdomoni na maradhi ya kisukari ukatokana na sababu kwamba meno yanapooza, husababisha uvimbe unaohusishwa na ukinzani wa insulin na kuchipuka kwa maradhi ya kisukari.

Kuvimba ni njia ya kawaida ya mwili kupigana na maradhi yanayowakumba watu. Shughuli hii inahusisha seli nyeupe za damu na bidhaa zinazozizalisha ili kuulinda mwili kutokana na maambukizi ya viumbehai kama vile bakteria na virusi. Kwa mfano watu wanapokosa kusugua meno, bakteria kwa kawaida hujikusanya na kufanya fizi zao ziwe katika hatari ya kukumbwa na maambukizi.

Ili kuangazia changamoto hii, mfumo wa kinga mwilini kwa kawaida huingilia kati na kukabiliana na maambukizi hayo. Hii husababisha ufizi kuvimba.

Muda unavyozidi kusonga na ikiwa maambukizi haya hayatadhibitiwa, uvimbe pamoja na kemikali unazozalisha vyaweza kusababisha maradhi mabaya ya ufizi kwa jina periodontitis; ugonjwa unaoonekana kudhoofisha uwezo wa mwili kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu.

Wakati wa utafiti huu, waandishi wakiwa ni pamoja na Dkt Tae-Jin Song kutoka Hospitali ya Seoul na Chuo Kikuu cha Ewha Woman’s University College of Medicine – walichanganua data zilizokusanywa kutoka kwa watu 188,013 kati ya mwaka wa 2003 na 2006 kupitia mfumo wa bima ya afya nchini Korea Kusini.

Watu hawa walikuwa na data kamili ya demografia, historia ya kiafya, viashirio vya usafi wa mdomoni au uchunguzi wa maabara.

Watafiti hawa walipata taarifa kuhusu mazoea yao kuhusiana na usafi wa mdomoni (ni mara ngapi walipiga mswaki, mara ngapi walimtembelea daktari wa meno kwa sababu yeyote na kusafishwa meno), vilevile idadi ya meno yaliyong’oka.

Mwishowe, waligundua kwamba asilimia 17 (takriban mmoja kati ya watu sita) ya washiriki katika utafiti huu waliougua maradhi ya periodontal, baada ya kufuatiliwa kimatibabu katika kipindi cha miaka 10, maradhi ya kisukari yaliwakumba watu takriban 31,545 (asilimia 16).