Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Anataka kunioa baada ya wazazi kututenganisha

March 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nilikuwa na mpenzi niliyempenda sana na alikuwa ameahidi kunioa. Hata hivyo, wazazi wake walipinga mpango wetu licha ya kwamba tulikuwa tumezaa mtoto pamoja. Badala yake walimtafutia mwanamke mwingine akamuoa. Huu ni mwaka wa tatu tangu alipooa na nilikuwa nimeanza kumsahau. Juzi alinipigia simu akanisihi sana tukutane na nikakubali. Tulipokutana aliniambia amegundua kuwa mke wake hawezi kupata watoto na ameamua kuoa mke wa pili. Aliniambia kuwa bado ananipenda na nikikubali atanioa mimi. Nishauri.

Kupitia SMS

Uamuzi wako kuhusu ombi lake utategemea mambo kadhaa. Muhimu zaidi ni iwapo wewe pia bado unampenda na uko tayari kuolewa mke wa pili. Kama ndivyo, jambo la pili la kuzingatia ni iwapo ameshauriana na kukubaliana na mke wake kuhusu mpango wake huo. Ni muhimu pia ujue iwapo wazazi wake watakubali kwa sababu walikukataa hapo awali.

 

Anadai ninayempata naye ni mwanafunzi mwenza eti hamna lolote, nimwamini?

Kwako shangazi. Nina mpenzi ambaye anasoma katika chuo kikuu. Nimemtembelea mara kadhaa na kumpata na mwanamume mwingine nyumbani kwake. Nilimuuliza akaniambia wanafanya kozi moja na kuwa hakuna chochote kati yao, huwa wanasaidiana kimasomo tu. Je, nimwamini?

Kupitia SMS

Inawezekana kwa mwanamume na mwanamke kushirikiana kwa karibu bila uhusiano wa kimapenzi kati yao. Hiyo hasa ndiyo hali ya kawaida katika sehemu nyingi za kazi. Hali hiyo pia inapatikana miongoni mwa wanafunzi kwa hivyo huna sababu ya kumshuku mpenzi wako. Iwapo unashuku kuna kitu kinachoendelea kati yao, chukua muda wa kutosha uchunguze ili ujue ukweli.

 

Angali anawasiliana na mpenzi wake wa zamani, nifanyeje?

Hujambo shangazi? Nilipendana na mwanamke fulani muda mfupi baada ya yeye kuachana na mpenzi wake. Huu sasa ni mwaka wa pili tukiwa pamoja. Ingawa ananiambia ananipenda, ninashuku kuwa hajaachana kabisa na huyo wa awali. Juzi nilipata fursa ya kukagua simu yake na nikapata mawasiliano kati yao lakini sijamuuliza. Nishauri.

Kupitia SMS

Hata kama mawasiliano kati yao hayahusu mapenzi, ni wazi kuwa wawili hao wako katika uhusiano mzuri na hiyo ni hali ya kutia wasiwasi ikizingatiwa kuwa walikuwa wapenzi. Mawasiliano ya aina hiyo yanaweza kuchochea tena hisia za kimapenzi kati yao na kuwafanya warudiane ama kuwa na uhusiano wa pembeni. Usipoziba ufa sasa utakuja kujenga ukuta. Itakuwa vyema umkabili mpenzi wako akwambie kinachoendelea kati yao ili uwe na hakika kuhusu mwelekeo wa mapenzi yenu.

 

Ameamua kuolewa na kuniacha hoi sijui sasa nitafanyeje kwani nampenda

Shikamoo shangazi! Mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu amenivunja moyo. Alihamishwa kufanya kazi mji mwingine miezi miwili iliyopita na tangu hapo akakatiza mawasiliano. Nimempigia simu mara nyingi na kumtumia jumbe za SMS bila majibu. Hatimaye, wiki iliyopita alinitumia SMS kuniambia ameolewa. Hatua yake hiyo imeniacha hali mbaya. Ninashindwa kulala na pia sina hamu ya chakula. Nahofia muda si mrefu nitaingiwa na wazimu. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Jinsi tu mapenzi yanavyokuwa matamu wahusika wakiwa pamoja, ndivyo yanaweza kugeuka machungu wakiachana. Hali unayopitia inatokana na kwamba mwanamke ambaye umempa moyo wako wote amekuacha ghafla kwa ajili ya mwanamume mwingine. Lakini usiruhusu hatua yake hiyo kuponza maisha yako. Jipe moyo na kukubali ukweli kuwa uhusiano kati yenu umekwisha kwa sababu sasa huyo ni mke wa mtu. Hali hiyo ni ya muda tu, hatimaye itatoweka na uweze kupenda tena.