• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
CORONA: Mechi zote za ligi ya Super8 zasitishwa

CORONA: Mechi zote za ligi ya Super8 zasitishwa

Na CHRIS ADUNGO

LIGI zote za Super8 zinazoendeshwa na Extreme Sports zimesitishwa humu nchini kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Mbali na hatari ya kusambaa kwa maambukizi ya corona, kuahirishwa kwa michuano hiyo pia kumechochewa na ukosefu wa mdhamini na hali ngumu ya kifedha ambayo kwa sasa inawakabili washiriki. Haya ni kwa mujibu wa kinara wa kipute hicho, Athanas Obala.

“Tumepania kuchangia makuzi ya vipaji vya chipukizi katika ulingo wa soka. Kwa sababu hiyo, tutajikakamua kutafuta mdhamini haraka iwezekanavyo,” akasema Obala kwa kusisitiza kwamba vipute vya Extreme Sports vitarejelewa hivi karibuni kwa malengo ya kupanua zaidi ushiriki wa baadhi ya ligi.

Wakati uo huo, Afisa Mkuu wa KPL Jack Oguda amesema kwamba kuahirishwa kwa raundi tatu zijazo za kinyang’anyiro cha msimu huu kutatiza pakubwa kalenda ya mpira wa soka.

Kwa mujibu wa Oguda, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lilikuwa limepanga kivumbi cha KPL kutamatika rasmi mnamo Mei 24 ili kupisha maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League) na Kombe la Mashirikisho (CAF Confederations Cup).

“Kusimamishwa kwa KPL kunamaanisha kwamba tutahitalifiana na kalenda ya CAF. Ilivyo, mpangilio wote wa michuano ya muhula huu umeathiriwa kwa kuwa hata mechi nyingi za kimataifa zimeratibiwa upya,” akasema.

Japo tarehe mpya ya kurejelewa kwa KPL ni Aprili 4 Oguda ameshikilia kwamba hana uhakika iwapo msambao wa virusi vya corona utakuwa umedhibitiwa vilivyo.

Kufikia sasa, CAF imeahirisha mechi zote za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021. Michuano yote 48 iliyokuwa itandazwe kati ya Machi 25-31 imesitishwa kwa muda usiojulikana licha ya visa vya maambukizi kufikia sasa kuripotiwa katika mataifa machache tu barani Afrika.

“Wachezaji mbalimbali waliotarajiwa kunogesha michuano ya kufuzu kwa fainali za AFCON wanachezea katika baadhi ya nchi ambazo zimeathiriwa pakubwa na virusi vya corona barani Ulaya na Asia,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo ya CAF kwa mashirikisho yote wanachama wa soka ya bara Afrika.

Isitoshe, CAF ilieleza kwamba serikali nyingi za mataifa ya bara Afrika zimetoa masharti makali na kanuni mpya zinazodhibiti usafiri wa raia wao huku baadhi ya nchi zikihitaji wasafiri wapya kutoka bara Ulaya kutengwa kwa muda wa hadi siku 14.

Awali, CAF ilikuwa imeshikilia kwamba ratiba yao ya soka ya bara Afrika ingalisalia kuwa jinsi ilivyokuwa imepangwa mwaka huu hadi wakati ambapo taifa fulani mwanachama wao lingaliripoti visa vya kuathirika zaidi kutokana na homa kali ya corona.

Ingawa serikali za nchi nyingi zimeandikia CAF zikitaka mechi zote kusitishwa, hakuna tarehe mpya ambayo imetolewa kwa mataifa hayo kuhusu siku ya kuandaliwa upya kwa mechi zilizosimamishwa.

Mechi nyingine za soka ya Afrika ambazo zimeahirishwa ni zile za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana wasiozidi umri wa miaka 20 na Kombe la Afrika (AFCON) 2020.

Michuano ya CHAN iliyokuwa isakatwe kati ya Aprili 4-25 nchini Cameroon pia imefutiliwa mbali.

  • Tags

You can share this post!

Mataifa 27 barani Afrika pia yaathiriwa na corona

Messi afarakana tena na uongozi

adminleo