• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Messi afarakana tena na uongozi

Messi afarakana tena na uongozi

Na MASHIRIKA

BARCELONA, UHISPANIA

KWA mara ya pili mwanasoka nyota Lionel Messi wa Barcelona amevurugana na uongozi wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uhispania (LaLiga).

Raia huyo wa Argentina ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, alianza kukwaruzana na Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo, Eric Abidal aliyeshutumu wachezaji kwa kutojitolea na kusababisha kutimuliwa kwa kocha Ernesto Valverde.

Akimjibu, Messi alimwita bosi huyo muongo mkubwa kwa kuwa alishindwa kutaja majina ya wale waliokuwa wazembe kikosini.

Lakini mara hii, ni Messi aliyeamsha vurugu akidai kwamba hana mpango wa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuchezea klabu hiyo ya Catalunya.

Messi amesema ameamua kuondoka baada ya wakuu wa klabu hiyo kushindwa kukamilisha usajili wa rafikye wa dhati Neymar Junior anyechezea klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa.

Kutokana na kuchelewa huko, Messi amewaambia wazi viongozi wa klabu hiyo kwamba haoni haja ya kuendelea kuwepo pale Camp Nou.

“Kwa sasa hatuna sababu ya kutufanya tunyakue ubingwa wa Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA). Kwa sasa sitatosheka na kiasi chochote kitakachowekwa mezani kunifanya nikubali mkataba mpya.”

Msimamo wa staa huyo mwenye umri wa miaka 32 umekuwa mtihani mgumu kwa Rais wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu, kwani ni majuzi tu mashabiki walipoanzisha maandamano ya kumtaka ajiuzulu.

Bartomeu alimshawishi Messi akubali mkataba mpya mnamo 2017, lakini safari hii itakuwa vigumu iwapo atashindwa kumleta klabuni Neymar.

Messi ana ushawishi mkubwa pale Barca ambao awali ulimfanya aliyekuwa mkurugenzi wao, Javier Faus kupoteza kazi kwa ajili yake.

Hii ni baada ya Faus kuropoka kwamba hawana haja ya kumpa Messi mkataba mpya, kauli ambayo ilimkera mshambuliaji huyo mahiri, ambapo hazikupita wiki nyingi kabla ya kiongozi huyo kupoteza kazi yake.

Mnamo 2016, alisikitisha vilivyo klabu hiyo alipotishia kutimka kwa madai kuwa hakuwa akiipigania viliyo timu hiyo wakati wa kashfa yake ya ukwepaji kodi lakini akaghairi nia baadaye.

Wakati huo huo, Juventus inajiandaa kumrejesha kiungo Paul Pogba wa Manchester United pale Turin.

Kadhalika, vigogo hao wa Serie A wanapanga kumvutia kiungo Sandro Tonali wa Brescia, na Hussem Aouar wa Lyon.

Tonali mwenye umri wa miaka 19 amevutia timu nyingi maarufu barani Ulaya baada ya kucheza mechi 23 za Serie A.

Aouar ni kiungo wa kimataifa wa timu ya Ufaransa ya wanasoka wasiozidi umri wa miaka 21, ambaye tayari ameichezea Lyon mara 37 katika mashindano tofauti msimu huu, ambako amefunga mabao tisa na kutoa pasi saba zilizochangia mabao.

  • Tags

You can share this post!

CORONA: Mechi zote za ligi ya Super8 zasitishwa

COVID-19: Bunge laahirisha vikao vyake hadi Aprili 14

adminleo