CORONA: Visa vyafika 7, jela kwa watakaokataa kujitenga
Na BENSON MATHEKA
Idadi ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini imeongezeka hadi watu saba huku waziri wa afya Mutahi Kagwe akionya Wakenya wanaorejea nchini kutoka ng’ambo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria wakikosa kujitenga kwa siku 14.
Watu watatu zaidi walithibitishwa kuwa na virusi hivyo Jumatano, wawili wakiwa raia wa Kenya waliozuru Ulaya mapema mwezi huu na mmoja akiwa raia wa Burundi. Mnamo Jumanne, serikali ilitangaza kuwa Wakenya wanne walikuwa wameambukizwa virusi hivyo.
Jumatano, Waziri Kagwe alisema kwamba raia huyo wa Burundi aligunduliwa kuwa na virusi hivyo katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi alipowasili kutoka Dubai.
“Hii inathibitisha yale ambayo nimekuwa nikisema, kwamba tuko na uwezo wa kukagua na kutambua kisa chochote cha corona,” alisema.
Bw Kagwe alieleza kuwa visa vya corona vilivyothibitishwa nchini ni kwa watu waliotoka ng’ambo.
Alisema Wakenya wawili waliopatikana na virusi hivyo ni wanandoa waliorejea Kenya Machi 5 baada ya kuzuru Madrid, Uhisipania.
Bw Kagwe alisema kuwa Wakenya wanaorudi nyumbani kutoka mataifa hayo ndio tishio kuu kwa wengine kwa kukosa kujitenga na kuonya kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria.
“Usipojitenga mwenyewe basi tutakutenga kwa nguvu katika kituo cha serikali na kukufungulia mashtaka ufungwe jela kwa kutishia afya ya umma,” Bw Kagwe alisema alipotoa taarifa ya wizara ya afya kuhusu hali ya corona nchini.
Aliwataka Wakenya kuripoti kwa maafisa wa serikali wakiona watu wanaokosa kujitenga baada ya kurejea nchini.
Waziri alisema kuwa Wakenya wote wanaorejea nchini baada ya kuzuru ng’ambo watakuwa wakijaza fomu wakiwasili katika uwanja wa ndege wakikubali kujitenga na kuchukuliwa hatua za kisheria wakikosa kufanya hivyo.
Bw Kagwe alisema Wakenya 18 wamelazwa katika hospitali ya Mbagathi jijini Nairobi, watu saba walipimwa na wakapatikana bila virusi hivyo.” Tunasubiri matokeo ya wengine 11,” alisema.
Waziri Kagwe alisema serikali inaendelea kufuatilia hali ilivyo nchini na ikiwa italazimu kufunga baadhi ya huduma na maeneo haitasita kufanya hivyo.
“Tutasimamisha huduma awakati kamati ya kitaifa itaamua inafaa kufanya hivyo. Hatutafanya maamuzi kwa misingi ya hisia tu,” alisema.
Hata hivvyo alihimiza Wakenya kufuata maagizo ya serikali ya kuepuka kukusanyika, kudumisha hali ya juu ya usafi kwa kuosha mikopo kila mara ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.