SEKTA YA ELIMU: Athari za kufungwa kwa shule zitakuwa kubwa mno kwa elimu
Na CHARLES WASONGA
KUSITISHWA kwa shughuli za masomo shuleni na vyuoni nchini kama sehemu ya hatua za kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kutaathiri pakubwa masomo mwaka 2020.
Watakaoathiriwa zaidi ni wanafunzi wa darasa la nane na wale wa kidato cha nne ambao wanajiandaa kwa mitihani ya kitaifa itakayoanza Novemba.
Kufungwa ghafla kwa shule kwa muda usiojulikana, bila shaka, kumevuruga ratiba ya masomo ya walimu ambao wanawaandaa wanafunzi wa darasa la nane kwa mtihani wa kitaifa wa KCPE.
Katika shule za upili, mipango ya walimu ya kuwatayarisha wanafunzi wa kidato cha nne kwa mtihani wa KCSE imevurugwa na hatua ya serikali kuamuru wanafunzi warejee nyumbani wiki nne kabla ya muhula wa kwanza kukamilika.
Kimsingi, walimu wa watahiniwa, hupania kukamilisha silabasi katika mihula ya kwanza na ya pili. Wao hutumia muhula wa tatu, ambao huwa mfupi mno, kuwapa nafasi wanafunzi kudurusu ili kuwaweka katika nafasi bora zaidi ya kupata matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa.
Kwa mfano, walimu na watahiniwa wa shule zilizopata matokeo bora katika mtihani wa KCSE walitaja kukamilisha mapema silabasi kama mojawapo ya sababu zilizowawezesha kufanya vizuri.
Kwa mujibu wa kalenda ya masomo ya mwaka wa 2020 iliyotolewa na Wizara ya Elimu mwishoni mwa mwaka jana, muhula wa kwanza ulipasa kuanza mnamo Januari 6, 2020 na kukamilika mnamo Aprili 14, kwa wanafunzi wa shule za chekechea, shule za msingi na zile za upili.
Muhula wa pili uliratibiwa kuanza Mei 4 hadi Agosti 7 huku muhula wa tatu ukianza Agosti 31 hadi Novemba 30.
Muhula wa kwanza na wa pili ulitarajiwa kudumu kwa wiki 14 huku masomo katika muhulu wa tatu yakiendeshwa kwa wiki tisa pekee ili kutoa nafasi kwa watahiniwa kufanya mitihani ya kitaifa.
Kwa mujibu wa kalenda hiyo, mtihani wa KCPE ulipangwa kuanza Novemba 2 hadi Novemba 5 huku ule wa KCSE ukidumu kwa majuma matatu kuanzia Novemba 6 hadi Novemba 30.
Likizo fupi katika mihula ya kwanza na pili ilipasa kuwa Februari 17 hadi 20 na Juni 15 hadi 19, mtawalia. Muhula wa tatu kwa kawaida hauwi na likizo fupi.
Sasa utaratibu huu wa shughuli za masomo shuleni hautazingatiwa ilivyopangwa baada ya kufungwa kwa shule kwa hofu ya kusambaa kwa virusi vya Korona.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (Kessha) Kahi Indimuli anaungama kwamba hatua hii itaathiri pakubwa ratiba ya masomo, japo ni muhimu.
“Bila shaka amri ya kufungwa kwa shule imehitilafiana na mipango yetu ya masomo. Lakini ni hatua muhimu kwa sababu itasaidia kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu hatari,” asema.
“Baada ya kugunduliwa kwa visa vitatu vya maambukizi ya virusi hivyo nchini, tuliomba kwamba shule zifungwe. Hii ni kwa sababu virusi hivyo vinaweza kusambaa kwa haraka zaidi katika taasisi kama hizi zenye wanafunzi wengi kupita kiasi baada ya serikali kutekeleza sera ya kuhakikisha wanafunzi wote waliofanya mtihani wa KCPE wanajiunga na shule za upili,” aliongeza Bw Indimuli ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Machakos.
Naye mwalimu mmoja wa ambaye aliomba tulibane jina lake alielezea hofu kwamba kusitishwa huko kwa masomo kutaathiri matokeo, haswa katika mtihani wa KCSE.
Aidha, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) Akelo Misori amelitaka Baraza la Kitaifa la Mitihani (Knec) na Wizara ya Elimu kusongeza mbele tarehe za kuanza kwa mitihani ya KCPE na KCSE.
“Kusongezwa kwa tarehe za kuanza kwa mitihani ya kitaifa kutawapa walimu na watahaniwa nafasi ya kujiandaa,” anasema Bw Misori.