AKILIMALI: Kijana anayevuna noti nzito ya zao la karakara
Na SAMMY WAWERU
UASIN Gishu ni miongoni mwa kaunti tajika katika uzalishaji wa nafaka eneo la North Rift. Ni kapu la mazao kama vile mahindi, ngano na maharagwe, ambayo mavuno yake huwa mara moja kwa mwaka.
Aghalabu wakulima hulalamikia bei duni ya mazao, juhudi zao za kujaribu kuishawishi serikali kuiimarisha zikionekana kuambulia patupu. Si kisa kimoja au viwili, wakulima eneo hilo wameonekana kulilia kiongozi wa taifa, wakimsihi ajali maslahi yao. Wakijaribu kusawazisha hesabu; mapato na gharama hususan ya pembejeo, faida wanayopokea ni kiduchu, wengine wakikadiria hasara tupu.
Licha ya masaibu hayo, hawana budi ila kuyavumilia; wanavyosema wajuvi, ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga; wana majukumu na mahitaji mengi ya kukidhi.
Katika kaunti hiyo, kwa sasa wakulima wanajibidiisha kuandaa mashamba kwa minajili ya upanzi, shughuli inayoshika kasi kati ya mwezi Machi hadi Mei.
Mengi ya mashamba, udongo ukiendelea kucharazwa na miale ya jua, katika mgunda wa kijana Alex Kandie katika kijiji cha Manyatta, Moiben, utalakiwa na rangi ya kijani cha matunda aina ya karakara.
Mikarakara ipatayo 800 na inayoendelea kuchumwa matunda imesitiriwa na ekari moja.
“Kilimo cha mahindi na ngano kina changamoto nyingi hasa soko ambalo linaendelea kuhangaisha wakulima. Niliamua pandashuka za aina hiyo hazitanikosesha lepe la usingizi. Moyo wangu umetulizwa na ukuzaji wa karakara,” akitabasamu aeleza Alex, adokeza kwamba ni kilimo-biashara alichokiingilia miaka miwili iliyopita.
Ni mhitimu wa Stashahada ya Habari na Teknolojia (IT) kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT). Alifuzu mnamo 2015 na kulingana na simulizi yake kupata ajira ilikuwa mithili ya kumtafuta paka mweusi kwenye giza totoro bila kurunzi.
“Kazi ya kushughulikia mitambo niliyopata katika kampuni moja ya ulinzi jijini Nairobi, niliifanya kwa muda mfupi, mwaka 2018 nikaingilia kilimo cha karakara, ambacho sijutii kamwe,” anaiambia Akilimali.
Hatua ya kuigura anasema ilichochewa na ziara aliyofanya katika shamba la rafikiye aliyekuza karakara kwenye ekari mbili, na anayeeleza kuwa pia aliacha kazi iliyomlipa maelfu ya pesa.
“Rekodi ya mauzo ilidhihirisha wazi aliogelea kwenye bahari ya pesa. Aliniambia mapato yalikuwa maradufu ya mshahara aliolipwa alipokuwa ameajiriwa,” Alex asema.
Hata ingawa hakufanya uamuzi mara moja, alirejea akiwa na wazo “sitaendelea kuwa mtumwa wa kazi yenye presha, msongo na mshahara usiokidhi mahitaji yangu”.
Anaendelea kueleza kwamba swahibu yuyo huyo ndiye aliyemnoa bongo namna ya kukuza matunda hayo, ambayo kwa sasa ni mithili ya dhahabu.
“Ilinigharimu mtaji wa Sh10, 000 pekee kuingilia kilimo cha karakara, ambazo nilikuwa nimeweka kama akiba,” akasema wakati wa mahojiano.
Kiasi kikubwa cha mtaji huo kilitumika kununua miche, mmoja akiuziwa kati ya Sh8- 10.
Hata hivyo, sasa hivi amebobea ambapo anajioteshea mbegu kupata miche, jambo analosema limempunguzia gharama.
“Ninachogharimia ni fatalaiza ya kuimarisha mazao, dawa ya wadudu na magonjwa na leba,” aeleza, akiongeza kuwa ana vibarua wawili.
Baada ya upanzi, mikarakara huchukua karibu miezi sita kuanza kuzalisha matunda.
Alex, 25, anasema wiki ya kwanza alivuna kilo 20, kiwango ambacho kimeongezeka hadi kufikia kilo 240 kwa sasa kila wiki.
Wataalamu wanasema muhimu katika ukuzaji wa matunda ni utunzaji kwa kutumia njia ya mbolea, fatalaiza ya kunawirisha na maji kwa wingi.
“Mfumo wa unyunyiziaji mashamba maji kwa mifereji unasaidia pakubwa katika kuimarisha sekta ya kilimo. Karakara huhitaji maji ya kutosha. Si ajabu, ukizingatia vigezo faafu, ekari moja kila wiki ikutuze zaidi ya kilo 800,” Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo cha matunda na miti anasema.
Usafi kwa njia ya palizi, Mwenda anasema, unasaidia kudhibiti usambaaji wa wadudu na magonjwa. Pia anahimiza haja ya kupogoa matawi na majani katika mikarakara, ili kuyapa matunda nafasi ya kupokea miale ya jua. Isitoshe, hatua hiyo pia inapunguza ushindani wa lishe; mbolea na maji.
Mkulima Alex anasema kilo moja ya karakara inanunuliwa kati ya Sh60 – 70, na kwa kuvuna kilo 240 kila wiki ina maana kuwa kijana huyo anatia kibindoni Sh14, 400, kiwango cha chini, mapato hayo yakikokotolewa kwa mwezi ni sawa na Sh57, 600.
Anadokeza kwamba gharama ya matumizi kila wiki huwa Sh2,500.
“Awali nilipoingilia kilimo cha karakara, kilo ilinunuliwa zaidi ya Sh100. Mawakala ndio wameharibu soko. Hata hivyo, baada ya siku nikifanya hesabu ninachosalia nacho ni faida tupu, ikilinganishwa na mshahara wa Sh25, 000 niliopokea katika ajira,” anafafanua.
Anasema ameongeza ekari moja zaidi kuzalisha karakara, ambapo anatazamia kufikia mwishoni mwa mwaka huu atakuwa akitia mfukoni Sh100, 000 kwa mwezi.
“Ekari moja inasitiri mikarakara kati ya 800 – 1,000, tayari nimepanda miche 1000,” asema.
Akisifia kilimo cha matunda hayo, anasema hakina ugumu wowote katika upanzi.
Huandaa mashimo ya kipimo cha futi mbili urefu, na kipenyo cha kimo sawa na hicho.
Aidha, nafasi kati ya mashimo anasema huipa mita mbili hadi tatu, mistari ya mashimo nayo akipendekeza isipungue mita tano.
“Hupanda kwa mbolea ya ng’ombe au mbuzi, ambao huwafuga,” anaeleza mkulima huyo.
Ana shimo lenye kimo cha futi 32, na pia hutegemea maji ya mvua. Maji yanapoadimika, msimu wa kiangazi, matunda hayo hayazalishi.
“Maji yakiwapo kwa wingi, mikarakara huchana maua na kutunda,” aeleza. Hunawirisha mazao kwa fatalaiza na mbolea.