Habari

Wanajeshi wa KDF waua al-Shabaab 12 na kumkamata mmoja akiwa hai Boni

March 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na KALUME KAZUNGU

JESHI la Kenya (KDF) limefaulu kuwaua washukiwa 12 wa al-Shabaab na kumshika mmoja akiwa hai katika eneo la Nginda, kati ya Korisa na Bar’goni katika msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu.

Katika ujumbe wake kwa Vyombo vya habari, Kamanda wa Jeshi linaloongoza Operesheni ya Linda Boni, David Chesire, alisema bunduki tatu aina ya AK47, maganda saba yaliyotumika ya risasi na risasi zenyewe zaidi ya 1,000 zilipatikana wakati wanajeshi wa KDF walivamia mojawapo ya kambi ya wapiganaji hao kwenye msitu huo wa Boni.

Pochi pamoja na kifaa maalum cha kubebea maji vilivyokuwa vikitumiwa na wapiganaji hao pia vilipatikana wakati wa uvamizi huo uliotekelezwa Alhamisi asubuhi.

Miongoni mwa waliouawa ni kamanda wa kundi hilo la al-Shabaab ambaye amekuwa akitoa usaidizi wa kijasusi kwa wapiganaji hao ukanda wa pwani na pia kuwasaidia katika shughuli za kimiundomsingi wapiganaji ambao wamekuwa wakiendeleza harakati zao ndani ya msitu wa Boni.

Kanali Chesire alieleza kuwa shambulizi hilo la KDF kwa kambi ya al-Shabaab ni katika harakati za kujibu jaribio la shambulio la kigaidi katika kambi ya KDF wa kitengo maalum eneo la Kotile.

Shambulio hilo la al-Shabaab lilitekelezwa mnamo Machi 13, 2020.

“Wanajeshi a kitengo maalum cha KDF wamefaulu kuwaua wapiganaji 12 wa al-Shabaab katika uvamizi wa kambi yao iliyoko Nginda kati ya Korisa na Bar’goni,” akasema Kanali Chesire kwenye ujumbe wake.

Kufuatia shambulio na mauaji ya wapiganaji hao, KDF wameongeza msako wa kuwatafuta magaidi zaidi ambao wanaaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni kwenye maeneo ya Lamu, Tana River na pia Garissa.

Bw Chesire alisema wanajeshi hawatalegeza kamba katika operesheni ya Linda Boni ambayo imekuwa ikiendelea katika kipindi cha zaidi ya miaka sita sasa.

Operesheni hiyo ilizinduliwa na serikali mnamo Septemba 2015 dhamira kuu ikiwa ni kuwafurusha au kuwamaliza wapiganaji wa al-Shabaab wanaoaminika kujificha kwenye msitu wa Boni.