• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:25 PM
‘Olimpiki ya mikosi’ Japan ikinusa jinamizi la miaka 40

‘Olimpiki ya mikosi’ Japan ikinusa jinamizi la miaka 40

Na MASHIRIKA

TOKYO, Japan

NAIBU Waziri Mkuu wa Japan, Taro Aso amesema Olimpiki ya 2020 “imelaaniwa” huku presha ikizidi kwa wasimamizi kuahirisha michezo hiyo kutokana na janga la virusi vya corona.

Michezo hiyo imepangiwa kufanyika jijini Tokyo kuanzia Julai 24 hadi Agosti 9.

Hata hivyo, tisho la corona limezidi kuyumbisha mipangilio huku wadau mbalimbali wakisukuma kamati andalizi kuifutilia mbali.

Aso, ambaye ana historia ya kutoa matamshi makali, aliambia kamati moja ya bunge kuwa michezo ya Olimpiki imekuwa ikiathiriwa na matukio ya dunia kila baada ya miaka 40.

Japan ilipanga kuwa mwenyeji wa Olimpiki mwaka 1940, lakini Vita Vikuu vya Dunia vya Pili vikalazimisha michezo hiyo kufutiliwa mbali.

Miaka 40 baadaye, mataifa mengi yakiwemo Marekani, Uchina na Japan yalisusia Olimpiki mjini Moscow kulalamikia Muungano wa Usovieti kushambulia taifa la Afghanistan.

“Ni tatizo ambalo limekuwa likijirudia kila baada ya miaka 40. Ni Olimpiki iliyolaaniwa, na huo ndio ukweli mchungu,” Aso alisema.

Maafisa wa Japan na wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) wamekuwa wakisisitiza kuwa lazima makala hayo ya 32 yaendelee jinsi yalivyopangwa.

Lakini Aso, ambaye pia anashikilia wadhifa wa Waziri wa Fedha, alisema kuandaa michezo hiyo Julai/Agosti haitakuwa jambo la busara ikiwa mataifa mengine hayataweza kuwasilisha wanamichezo wao kwa mashindano.

“Jinsi Waziri Mkuu (Shinzo Abe) alivyosema, ni muhimu michezo ya Olimpiki ifanyike katika mazingira ambayo kila mtu anahisi yupo salama na pia anafurahia. Hata hivyo, Japan peke yake haiwezi kufanya uamuzi huo.”

Waandalizi wa michezo ya Tokyo 2020 walimtayarisha muogeleaji wa Japan aliyeshiriki Olimpiki ya 1996, kupokea mwenge wa michezo hiyo wakati wa sherehe ndogo ya mapokezi mjini Athens, Ugiriki hapo Alhamisi.

Naoko Imoto, ambaye anafanya kazi na Shirika la Kulinda Watoto Duniani (Unicef) alijaza pengo hilo baada ya vikwazo vya usafiri kutokana na corona kuzuia msafara wa Japan kuzuru Athens kupokea mwenge huo, ambao unatarajiwa kuwasili nchini Japan hii leo.

“Tuliamua jana (Jumatano) kuwa ilikuwa muhimu raia wa Japan afanye majukumu hayo,” afisa mkuu mtendaji wa kamati andalizi, Toshiro Muto aliambia wanahabari.

Mashindano hayo huleta pamoja mataifa 200. Hata hivyo, makala ya mwaka huu yamevurugwa na kuenea kwa virusi hatari vya corona, viliyoanzia Uchina mwezi Desemba na sasa vimesambaa katika mataifa zaidi ya 150.

Kufikia Alhamisi vifo zaidi ya 8,000 na maambukizi 200,000 yalikuwa yameripotiwa kote duniani.

You can share this post!

Wanajeshi wa KDF waua al-Shabaab 12 na kumkamata mmoja...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Kumcha Mungu kuna faida nyingi...

adminleo