Habari

COVID-19: Benki ya Family yaanza kutekeleza maagizo ya CBK

March 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

BENKI ya Family imetangaza Ijumaa kwamba imeanza kutekeleza utaratibu na maagizo yaliyotolewa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwa benki na mashirika yote ya kifedha nchini, kufuatia janga la Covid-19.

Kwenye taarifa kwa wateja wake, benki hiyo imesema itaongeza muda wa kuanza kulipa mikopo kwa waliochukua kuanzia Machi 2, 2020, kisa cha kwanza cha virusi vya corona kiliporipotiwa hapa nchini.

Mapema wiki hii, Gavana wa CBK Dkt Patrick Njoroge aliamuru benki zote nchini pamoja na mashirika ya kifedha kuongezea wateja waliochukua mikopo kuanzia Machi 2, 2020, muda wa hadi kipindi cha mwaka mmoja kuanza kuilipa.

Dkt Njoroge alitoa amri hiyo kufuatia hali ngumu wanayopitia wananchi kwa sababu ya hofu ya maenezi zaidi ya Covid-19, na ambayo yametatiza utendakazi na biashara nyingi nchini na hata kutikisa dunia kwa jumla, hasa mataifa yaliyotajwa kuathirika.

“Tutaongezea muda waliochukua mikopo kibinafsi, ya kuimarisha biashara ndogondogo na za kadri – SMEs na mikopo ya makundi, kwa waliochukua kuanzia Machi 2. Hatua hii itabainishwa na hali yako kwa sasa. Kwa maelezo zaidi wasiliana na meneja wa uhisiano mwema wa benki yako au tawi lolote la benki yetu iliyo karibu nawe,” inaeleza taarifa ya Afisa Mkuu Mtendaji wa Family Bank, Rebecca Mbithi.

Ikitoa hakikisho kwa umma kufuata utaratibu na masharti yaliyotolewa na serikali ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona, benki hiyo imesema imeweka jeli ya kunawa mikono katika matawi yake yote nchini, huku ikiwataka wateja kusafisha mikono kabla kuingia kuhudumiwa.

“Tumefanya mabadiliko kadha ya huduma zetu, wafanyakazi watawahudumia wakiwa nyuma ya kioo sehemu ya kaunta. Pia kigezo cha umbali wa mita moja kitatekelezwa,” Benki ya Family imearifu.

Aidha, ikieleza kusikitishwa na mahangaiko wanayopitia wananchi na wateja wake kufuatia hofu ya Covid – 19, benki hiyo imesema huduma zake kwa njia ya simu, apu ya Pesa Pap na mitandao zingali zinaendelea kama kawaida.

Imetangaza kuondoa ada zote mteja anapotaka kujua kiwango cha pesa alizonazo kwenye akaunti yake, kupitia kaunta au kwa njia ya simu.

Kwa maelezo zaidi, wateja wa Benki ya Family wamehimizwa kuwasiliana nayo kupitia nambari za simu: 0703095445 au kutembelea matawi yake.

Kwenye uchunguzi wa ‘Taifa Leo’, kufikia Alhamisi jioni idadi ya wateja waliozuru tawi la Family Bank, Githurai, ilionekana kuwa ya chini mno.