• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Gor haitapewa KPL iwapo ligi kuu haitatamatika rasmi – Oguda

Gor haitapewa KPL iwapo ligi kuu haitatamatika rasmi – Oguda

Na CECIL ODONGO

USIMAMIZI wa Kampuni Inayosimamia Ligi Kuu (KPL) umekanusha kwamba Gor Mahia watapokezwa taji la msimu huu iwapo janga la virusi vya corona litaendelea kuathiri taifa hili.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL, Jack Oguda, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, alisema kwamba hawajafikia uamuzi huo na itakuwa vigumu K’Ogalo kupokezwa taji ikizingatiwa mwanya wa alama kati yao na Kakamega Homeboyz na Tusker, ambao ni mdogo sana.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Barry Otieno alikuwa amenukuliwa na mtandao mmoja unaochapisha habari za spoti, akisema msimamo wa jedwali la sasa utatumika kuamua mshindi iwapo mechi za KPL hazitarejelewa.

“Kuna mechi 10 ambazo zimesalia kabla ya msimu kukamilika na kwa FKF kusema kwamba Gor watapokezwa taji na hawasimamii ligi ni jambo la kusikitisha. Hatujafanya uamuzi wa kupokeza K’Ogalo taji jinsi wanavyodai,” akasema Oguda.

Afisa huyo alisema kwamba iwapo hali itazorota zaidi huenda mshindi wa KPL akapatikana kulingana kanuni zilizowekwa na Shirikisho la soka duniani (FIFA) au kuiga jinsi ambavyo Ligi Kuu za Uingereza, Uhispania, Ujerumani na Ufaransa zitaamua mshindi wao.

“Tutashauriana na Fifa au kuiga ligi za bara Ulaya ambazo pia zimesimamishwa kutokana na corona. Aidha pia tutnweza kuamua kwamba timu mbili za kwanza zishiriki mchujo. Njia ni nyingi lakini si sahihi kusema kwamba tutapokeza Gor taji la msimu huu,” akaongeza.

Oguda pia alisema kwamba huenda wachezaji wakawa na muda mfupi wa kupumzika kabla ya msimu mpya kuanza Agosti, iwapo mapumziko ya sasa yataendelea kwa zaidi ya mwezi moja.

“Tutafakari kuhusu kujumuisha siku za sasa kama sehemu zile za mapumziko msimu ukiisha. Iwapo janga hili litazidi kwa zaidi ya mwezi moja basi, watalazimika kupumzika kwa siku chache ama kuanza tu msimu. Kwa sasa ni wazi kwa ratiba yetu imevurugika lakini mshindi wa KPL lazima apatikane,” akasema Oguda.

Matamshi ya Otieno, tayari yameshutumiwa na mwenyekiti wa Kakamega Homeboyz, Cleophas ‘Toto’ Shimanyula ambaye anasema timu yake haitakubali K’Ogalo ipokezwe ubingwa, akisisitiza iko katika nafasi nzuri ya kushinda taji hilo.

Shimanyula alidai kwamba wamebaki na wapinzani dhaifu ikilinganishwa na K’Ogalo na njia pekee ya kubaini mshindi wa KPL iwapo mechi hazitarejelewa ni Kakamega Homeboyz kuchuana na Gor kwenye uwanja usiokuwa na mashabiki.

  • Tags

You can share this post!

COVID-19: Benki ya Family yaanza kutekeleza maagizo ya CBK

ICJ: Wakenya wa mapato madogo waangaziwe pia

adminleo