AKILIMALI: Anatumia mkojo wa sungura kuimarisha kilimo cha nyanya mwitu

Na JOHN NJOROGE

njorogejunior@gmail.com

Joseph Maina Kanai hawezi kuwa na majuto alipojiondoa kwa ukulima wa mahindi miaka minne iliyopita na kuanza kilimo biashara katika nusu ekari ya shamba lake la Turi mjini Elburgon katika Kaunti ya Nakuru.

Akilimali ilipomtembelea katika shamba lake hivi majuzi katika barabara kuu ya Molo- Nakuru karibu na mji wa Elburgon, Maina aliyevalia suruali ndefu nyeusi iliyofanana na shati na pia buti nyeusi alikuwa ameshikilia ndoo ya rangi ya waridi huku akizunguka ndani ya shamba lake la nyanya mwitu (tree tomato), akiyaangalia matunda yaliyoiva.

Kando yake palikuwa na kifaa cha rangi ya manjano anachotumia kunyunyizia dawa.

Mkulima huyu anayevuna matunda haya kila baada ya majuma mawili, alisema kuwa alipanda miche mia nne za nyanya mwitu, alizozitumia baadaye kupanda katika sehemu yake ya shamba.

“Nilikuwa nimetenga robo ya shamba langu ambapo nilipanda nyanya mwitu,,’’ akasema Maina akiongeza kuwa miche zilizobaki aliwauzia wakulima wengine.

Alisema kuwa mwaka wa 2019 ulipoanza, alitumia shilingi 10,000 kwa mbolea na matayarisho ya shamba lake la nyanya mwitu.

Maina aliyetumia mbolea ya nyumbani kwa upanzi wake, alisema kuwa alifunga shina za matunda yake baada ya wiki mbili ili kuzuia urefu na utatanishi wa matunda hayo ifikapo nyakati za kuvuna.

“Wakati minyanya mwitu iliendelea kukua, ilipatwa na koga lakini nilinyunyizia kemikali ya kujitengenezea ambayo ni lita kumi ya maziwa,’’ akasema bwana Maina.

Baada ya mwezi mmoja au miwili tangu ayapandenyanya mwitu, alisema kuwa alinyunyinzia mkojo wa sungura kama mbolea ya mmea wake ambapo kulingana na Taasisi na Utafiti wa Ukulima nchini Kenya ina virutubisho kama vile naitrogeni na potasiamu inayosaidia kwa vyakula kunawiri.

Alitenganisha mita mbili kwa mbili alipopandanyanya mwitu iliyomwezesha kupanda vyakula vingine kwa mseto kama vile vitunguu, saladi, mchicha baadhi ya vyakula vingine.

Wakati wa kiangazi, mkulima huyu hunyunyizia mimea yake maji kutoka kwa matangi mawili makubwa yanayotoa maji kutoka kwa mto ulio karibu kwa kutumia pampu nyingi zilizojaa shambani lake la kilimo biashara.

“Matunda haya huvamiwa na wadudu weupe hasa kwa nyakati za kiangazi,’’ akasema na kuongeza kuwa yeye hunyunyizia kemikali ya kujitengenezea kama vile vitunguu saumu ili kuwaua na kuwafukuza wadudu hao.

Maina alikiri kuwa aliyapata mafunzo na teknolojia ya ukulima kutoka kwa semina na maonyesho ya kilimo aliyotembelea kwa wingi. Yeye pia hutembea katika chuo cha elimu na ukulima cha Baraka mjini Molo wakati wa siku ya wakulima ambapo wakulima hupata mafunzo mengi ya ukulima na utumizi wa mbolea.

“Mimi hupenda kutumia mbolea ya viumbe hai ama ya kujitengenezea ambayo hunipunguzia gharama na pia ni rahisi kuitengeneza,’’ akasema.

Wakati alikuwa ameajiriwa katika shamba moja la Maua mjini Elburgon, alisema kuwa alipata maarifa kadhaa kupitia kwa mtaalamu wa kemikali aliyekuwa akihudumu katika shamba hilo.

Katika mauzo ya matunda yake, Maina alisema kuwa kilo moja inauzwa kwa Sh80 katika soko la Top Market mjini Nakuru ambapo ana wateja wengi ambapo kila tunda moja huuza kwa shilingi kumi.

Kilio chake kikubwa ni kuwa bei ya nyanya mwitu haipandi hata wakati wa kiangazi ambapo hazipatikani kwa wingi.

Aliongeza kuwa fuko huvamia shamba lake na kumwezesha kutumia mtego ili kuwanasa fuko hao.

Msimamizi wa kilimo mjini Molo amewaomba wakulima kuripoti shida zozote zinazokuba mimea ama wadudu kabla ya kujitibia wenyewe.

Kabla ya mwaka kumalizika, mkulima huyu anatarajia kupata zaidi ya Sh100,000 kutoka kwa zao hilo ambalo alisema hawezi linganisha na zao la mahindi.

Alisema hakuna mkulima yeyote wa mahindi angeweza kuuza na kupata pesa kama hizo kutoka kwa robo ekari kama hiyo aliyopanda nyanya mwitu kati ya mwaka mmoja.

“Unaweza panda sehemu ndogo ya shamba na kupata pesa nzuri bila hata kutumia matumizi mengi,’’ akasema huku akitabasamu.

Kwa siku sijazo, Maina anatarajia kuongeza shamba lake la minyanya mwitu na kuwaajiri wafanyi kazi wengi. Kwa sasa, yeye hutumia Sh200 kila siku kwa mhudumu wa shamba lake.

 

Habari zinazohusiana na hii