Michezo

Dagoretti Mixed yalenga ushindi fainali za Chapa Dimba

March 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wavulana ya Dagoretti Mixed inalenga kutifua vumbi kali katika fainali za kitaifa za Chapa Dimba na Safaricom, Season Three msimu huu.

Ngarambe ya mwaka huu itaandaliwa mwezi Juni, mjini Mombasa ambapo itashirikisha timu nane za wavulana na saba za wasichana.

Dagoretti Mixed itashiriki kipute cha muhula huu kuwakilisha Mkoa wa Nairobi baada ya kuwapiku wapinzani wao kwenye fainali zilizopigiwa Uwanja wa Shule ya Upili ya Jamhuri mwezi uliyopita.

”Kusema kweli tunafahamu bayana fainali za raundi hii zitakuwa mambo mbaya kila timu itakuwa kazini kupigana kufa na kupona kuwania taji hilo,” kocha wa Dagoretti Mixed, Joseph Orao alisema na kuongeza kuwa timu nyingi zimekuwa zikijipanga kufanya kweli maana imegunduliwa mashindano haya yatakuwa yakiandaliwa kila mwaka.

Pia anasema wavulana wake wamo ng’ang’ari kukabili wapinzani wao kwa udi na uvumba kupigania taji hilo.

Lewis Mutava wa Hakati Sportiff anamzuia mwenzake wa Brookshine Academy kwenye mechi ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three katika Mkoa wa Nairobi. Picha/ John Kimwere

Kadhalika anasema ana imani Dagoretti Mixed inayo nafasi nzuri kuibuka ya kwanza katika Mkoa wa Nairobi kushinda taji hilo la kitaifa maana hakuna timu nyingine ya Niarobi iliyowahi kulishinda.

Dagoretti Mixed ilinasa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa ilipocharaza Hakati Sportiff kwa mabao 4-3 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.

Kwenye nusu fainali Dagoretti Mixed na Hakati Sportiff kila moja ilitwaa 3-0 dhidi ya KSG Ogopa na Brookshine Academy mtawalia.

Katika hali ya kushangaza wavulana sita waliibuka wafungaji bora baada ya kila mmoja kufungia timu yake bao moja kwenye fainali hizo.

Wao walikuwa Mongai James, Hagai Victor na Felix Okoth wote Dagoretti Mixed. Wenzao wa Hakati Sportiff wakiwa Bandi Lewis, Mutava Lewis na Otieno Juma.

Dagoretti Mixed ilishinda KSG Ogopa kimiujiza maana wengi waliamini KSG ingeibuka mabingwa wa Mkoa wa Nairobi.

KSG Ogopa ni miongoni mwa vikosi vinavyotesa kwenye kampeni za kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.

Kufikia sasa tayari timu za Mikoa kadhaa zimefuzu kushiriki kipute hicho zikiwamo: Laiser Hill (Mkoa wa Bonde la Ufa), Berlin FC (Mkoa Kaskazini Mashariki), Ulinzi Youth (Mkoa wa Kati), Dagoretti Mixed (Mkoa wa Nairobi), Tumaini School (Mkoa wa Mashariki) na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa. Timu itakayoshinda fainali za kitaifa itatuzwa kitita cha Sh1 milioni.