• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
AKILIMALI: Waanzisha kiwanda cha bishara ya nyama ya sungura

AKILIMALI: Waanzisha kiwanda cha bishara ya nyama ya sungura

NA RICHARD MAOSI

[email protected]

Wakulima wengi nchini hususan kutoka mashinani, wamekuwa wakijihusisha na ufugaji wa sungura bila kujua wanaweza kutengeneza hela nzuri, kutokana na kilimo biashara cha sampuli kama hii.

Kulingana na utafiti, asilimia kubwa ya mwili wa sungura umebeba nyama badala ya mifupa, kinyume na wanyama wengine kama vile kondoo, mbuzi na ngombe.

Aidha nyama ya sungura ni salama kwa walaji ambao mara nyingi huwa ni watoto au watu waliokonga kiumri, ambao meno yao hupata taabu wakati wa kula nyama.Pia manufaa ya nyama ya sungura kiafya ni mengi ikiwemo ni pamoja ya kupunguza shinikizo la damu mwilini.

Hali ni hiyo kwa Ben Njoroge mkaazi wa Thika ambaye ni mjasiria mali na msambazaji wa nyama ya sungura mjini Thika.Anasema biashara yenyewe haina mfano na anawahimiza wakulima wengine kujitosa katika kazi hii.

Sungura kutoka kwa wafugaji

Alianza mradi wenyewe mnamo 2019, akiwa na lengo la kuwaleta pamoja wakulima wadogo kutoka Thika, Kiambu, Muranga na Nyeri chini ya mwavuli mmoja wa kutafuta soko kwa sungura wao kimataifa.

Pia akiwa mwenyekiti wa Kenya Informal Traders Association (KITA) anasema anafanya kazi kwa ukaribu na taasisi za elimu kama vile chuo cha Jomo Kenyatta University of Science and Technology ili kuwahimiza vijana kujitosa kwa wingi katika kilimo ili waje kuwa watu wa kujitegemea siku za baadae.

Ben anasema aliwashauri wakulima wengi wanaokaa Thika , ambao awali walikuwa wakiendesjha kilimo kidogo katika makazi yao akilenga kuwazindua ili wawekeze pakubwa katika ufugaji wa sungura.

“Kufikia sasa ninafanya kazi na takriban wakulima 35 ambao wamejistawisha baada ya kupata elimu ya kutosha pamoja na mtaji wa kuanzisha biashara hii isiyokuwa na watu wengi humu nchini,”aliambia Akilimali.

Sungura wakipimwa uzani

Ben aliongezea kuwa sungura ni wanyama rahisi kufuga muradi mkulima ahakikishe wanahifadhiwa katika sehemu salama , mbali na mbwa mwitu au Wanyama hatari wanaoweza kuwadhuru.

Kulingana naye sungura wengi anaopata ni wale wa kienyeji, ambao mara nyingi ni wa manufaa makubwa ijapo katika soko la nyama.Aliongezea kuwa ingawa nyama ya sungura ni bei ghali inaweza kuchukua nafasi ya samaki au kuku (white meat).

Ben anasema serikali ya kaunti ya Kiambu ilitoa sehemu ya kichinjio bila malipo, katika eneo la Makongeni mwanzoni mwa 2019.Ilimlazimu Ben kutafuta friji na wafanyikazi wawili ambao wamekuwa wakimsaidia kuchinja kila siku ya Jumanne.

Aidha ili kuwainua wakulima Ben amekuwa akiwapatia wakulima sungura watano bila malipo, huku akiwatengenezea kibanda cha kuwahifadhi bila malipo na hatimaye yeye hutarajia kuwanunua sungura hao kutoka kwa wakulima kwa 3500 kila mmoja.

Hatua za kupokea sungura

Ben anasema kuwa mara ya kwanza yeye huwapokea sungura kutoka kwa wakulima kwa 3500 na wakati mwingine kuwauza kwa 4000.

Mara tu anapowapokea sungura yeye hupima uzani kabla ya kuwaweka ndani ya aina maalum ya kibanda kiband (cage), wakisubiri kuchinjwa kwa sababu bei ya sungura huwa inategemea uzani wake.

Hatimaye mara wanapochinjwa sungura husafishwa, kisha nyama ikakatwa vipandevipande ikahifadhiwa katika sehemu safi ikisubiri kusafirishwa katika maduka ya kijumla mengi yao ikiwa ni matawi ya Tuskys.

Kuboresha huduma kwa sungura

Mbali na kuwanunua na kuwauza sungura kwa wakulima wengine Ben analenga kufiki soko la kimataifa ambalo linahitaji nyama ya sungura kutokana na upungufu wa samaki katika maziwa makuu duniani.

Mbali na kutengeneza vibanda vya kulinda sungura, anahakikisha kuwa mkulima analipia sungura wake bima ili kuwakinga dhidi ya hatari hasa mkurupuko wa maradhi kama vile homa kali inayoweza kuzaka wakati wa baridi.

Pili anatumia huduma za kitaalam kutoka kwa madaktari wa mifugo wanaosaidia kutoa ushauri nasaha kuhusu mbinu mwafaka za kutunza sungura dhidi ya maradhi ya Pneumonia ama kuwapatia chanjo.

Ben Njoroge(Kushoto) pamoja na mwenzake wakionyesha wanavyotumia kuhifadhi nyama ya sungura mara tu baada ya kuchinjwa katika kichinjio cha Thika.

Anasema baada ya miezi mitatu sungura huwa wamepata ujauzito na mkulima atahitaji sungura wanne wa kike na mmoja wa kiume 4.1.Nao hujifungua baina ya vitoto 8-12.

“Kutokana na sungura wanne wa kike mkulima anaweza kupata takriban vitoto 32 katika kipindi cha miezi mitatu, kisha baada ya miezi mingine mitatu endapo sungura wa kike watakua ni 20 mkulima anaweza kupata vitoto 160,”aliongezea.

“Kwa kuwa mkulima hahitaji idadi kubwa ya sungura dume, wao hupelekwa kichinjio na kufanywa nyama huku wale wengine wanaosalia wakabaki kuendeleza kizazi,”akasema.

Kwa wiki moja Ben pamoja na wakulima wenzake wanaweza kupokea kilo 600 ya nyama, ingawa sehemu nyingine kama vichwa na miguu haziwezi kulika ila hutupwa.

Licha ya changamoto nyingi ambazo mkulima anaweza kupata wakati wa kufuga sungura katika hatua za mwanzoni, kilimo hiki endapo kitamkubali anaweza kutengeneza zaidi ya milioni moja au zaidi kila mwaka.

Aidha Ben ameanzisha kikundi cha wakulima ambao wao hutumia wakati wao mwingi kutembeleana na kujifunza namna sekta ya ufugaji inaendelea kubadilika kutokana na uhaba wa mashamba ya kuendesha kilimo hususan mijini.

Pia Ben anafanya kazi ya kuuza mbolea kutokana na mkojo wa sungura ambayo huwa na virutubishi vya kutosha kushinda mbolea za kawaida zinazopatikana viwandani.

Wahudumu katika kichinjio cha Makongeni wakiendelea kuchinja sungura, wanaopokea kila siku ya Jumanne kutoka kwa wakulima wa Kiambu.

You can share this post!

Asiya atashiriki Olimpiki Tokyo michezo ikiendelea

AKILIMALI: Ndizi ni uwekezaji wa maana, panda kwa wingi

adminleo