Habari

COVID-19: Kenya yathibitisha visa 9 vipya vya maambukizi idadi jumla ikifika 25

March 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

WAKENYA wamelaumiwa kwamba wengi wameonyesha utovu wa nidhamu, tabia ambayo ni pigo katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema hayo Jumanne wakati akitangaza maambukizi tisa mapya huku idadi ya walioambukizwa ikifika 25.

“Visa hivi vipya ni vya wagonjwa saba Wakenya na hao wengine wawili ni raia wa kigeni,” amesema waziri Kagwe.

Kulingana na Waziri Kagwe, wahudumu wa matatu na wazazi wa baadhi ya wanafunzi wameonekena kutofuata sheria zilizowekwa na serikali kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

“Jambo ambalo limejitokeza wazi wakati tunakabiliana na janga hili ni kwamba Wakenya wengi wana utovu wa nidhamu na hii ndiyo changamoto kuu,” amesema Bw Kagwe.

Waziri ameonekana kughadhabishwa na wazazi ambao wanawaruhusu watoto wao ‘kurandaranda’ mitaani na hivyo kuwa katika hatari ya maambukizi.

“Nia ya kuzifunga shule ilikuwa ni kuwafanya watoto wasalie nyumbani na wala sio kurandaranda,” ameongeza Bw Kagwe.

Mtaalamu wa hamasisho la kunawa mikono Dkt Myriam Sidibe ambaye ana shahada ya uzamifu katika ujuzi wa kunawa mikono ameonyesha jinsi ya kuosha kila sehemu ya mkono ipaswavyo.

Mtaalamu wa hamasisho la kunawa mikono Dkt Myriam Sidibe. Picha/ Magdalene Wanja

Waziri amesema kaunti zilizoathirika zaidi ni Nairobi, Mombasa, Kilifi, na Kwale.